ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

 

MJADALA JUU YA AYA YA KUKAMILISHA DINI
MJADALA JUU YA KAULI ISEMAYO: AYA YA KUKAMILISHA DINI ILISHUKA SIKU YA ARAFA'
Bukhari ameeleza ndani ya sahihi yake amesema: "Ametusimulia Muhammad bin Yusuf, ametusimulia Sufian kutoka kwa Qais bin Muslim naye toka kwa Tariq bin Shihab kuwa watu fulani miongoni mwa Mayahudi walisema, Lau aya hii ingeshuka kwetu basi siku hiyo tungeifanya kuwa sikukuu, Umar akasema, aya gani? Wakasema, "Leo nimekukamilishieni Dini yenu na nimekutimizieni neema yangu." Basi Umar akasema, "Mimi najua mno mahala gani ilishuka, ilishuka wakati Mtume akiwa amesimama Arafa". Taz: Sahih Bukhar Juz. 5 uk. 125.

Na amethibitisha Ibn Jarir kutoka kwa Isa bin Harithah Al-Ansari amesema: "Tulikuwa tumekaa ndani ya Ofisi, basi Mkristo mmoja akatuambia, Enyi Waislamu! hakika mmeshushiwa aya ambayo lau ingeteremshwa kwetu basi siku hiyo na saa hiyo (ilioteremshwa) tungeifanya kuwa ni sikukuu muda wote japo watabakia miongoni mwetu watu wawili, nayo ni ile aya isemayo: "Leo nimekukamilishieni dini yenu" Basi hapana yeyote miongoni mwetu aliyemjibu, nikakutana na Muhammad bin Kaab Al-Qurtubi nikamuuliza kuhusu jambo hilo akasema: "Hivi hamkumjibu"? Umar bin Al-Khatab alisema: "Ilishuka kwa Mtume hali ya kuwa amesimama juu ya mlima siku ya Arafah, basi haijaacha siku hiyo kuwa ni sikukuu kwa Waislamu muda wote ataobakia mmoja miongoni mwao". Taz: Ad-Durrul-Manthur Juz. 3 uk. 18.


Kwanza: Tunaona kwa kupitia riwaya hizi kwamba, Waislamu walikuwa hawajuwi tarehe ya siku hiyo kuu na wala Waislamu walikuwa hawasherehekei jambo ambalo liliwafanya Mayahudi kwa mara ile ya kwanza na Wakristo kwa mara nyingine tena wawaambie Waislamu: "Lau aya hii ingeshuka kwetu, basi siku hiyo iliyoshuka tungeifanya kuwa sikukuu." Hali hii ilimlazimisha Umar bin Al-Khatab aulize ni aya gani hiyo? Na waliposema: "Leo nimekukamilishieni dini yenu" Umar akasema hakika mimi najua mno mahala gani iliteremshwa, iliteremshwa hali ya kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) akiwa amesimama Arafah.

Kwa hakika sisi tunahisi kwamba kuna namna fulani ya utata na kuficha ukweli katika riwaya hii, na kwamba watu walioizua hadithi hii kupitia ulimi wa Umar bin Al-Khatab katika zama hizo za Bukhari walitaka kuafikiana na Mayahudi na Wakristo juu ya kwamba siku hiyo ni siku tukufu ni wajibu iwe sikukuu, na kwa kuwa wao Waislamu hawaisherehekei siku hiyo wala kuikumbuka japo mara moja mpaka wameisahau na wakati kinachotakiwa ni kuwa iwe miongoni mwa siku kubwa kwa Waislamu kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwakamilishia Dini yao ndani ya siku hiyo na akawatimizia neema yake na kuwaridhia Uislamu kuwa dini yao. Na kwa ajili hiyo utaona katika riwaya ya pili kauli ya msimuliaji pale alipoambiwa na yule Mkristo "Enyi Waislamu kwa hakika mmeteremshiwa aya ambayo lau ingeteremshwa juu yetu basi siku hiyo tungeifanya kuwa ni sikukuu japo watabakia watu wawili miongoni mwetu".


Msimuliaji amesema: "Hakuna yeyote aliyemjibu miongoni mwetu" Na hiyo ni kwa sababu ya kutokujua kwao tarehe na heshima ya siku hiyo na Utukufu wake. Inaonesha kwamba msimuliaji mwenyewe alishangaa ni kwa vipi Waislamu wanapuuza kusherehekea siku kama hiyo ndiyo maana tunamuona anapokutana na Muhammad bin Kaaba Al-Qurtuni na kumuuliza juu ya jambo hilo huyu naye anamjibu kuwa, "Umar bin Al-Khatab alisimulia kwamba aya hiyo ilishuka kwa Mtume (s.a.w.) akiwa amesimama kwenye mlima siku ya Arafah."

Kwa hiyo basi lau siku hiyo ingekuwa inajulikana kwa Waislamu kwamba ni sikukuu basi wapokezi hawa wasingekosa kuijua sawa sawa wakiwa ni miongoni mwa Masahaba au waliowafuatia Masahaba, kwani kilichothibiti na kinachojulikana kwao ni kwamba Waislamu wanasikukuu mbili tu nazo ni sikukuu ya mfunguo Mosi na sikukuu ya mfunguo Tatu mpaka hata wanachuoni na wanahadithi kama vile Bukhari na Muslim na wasiokuwa hao unawaona wanathibitisha ndani ya vitabu vyao, "Kitabul-Idain " (Yaani Mlango unaohusu sikukuu mbili) - (au) Sala ya Idi mbili na Khutba za Idi mbili na mambo mengineyo yanayokubalika kwao na kwa wengine lakini hakuna sikukuu ya tatu.


Dhana kubwa iliyopo ni kwamba wale wasemao juu ya misingi ya mashauriano kuhusu Ukhalifa na waasisi wa nadharia hii, wao ndiyo ambao waliogeuza kushuka kwa aya hiyo kutoka kwenye ukweli wake halisi, ambao ni siku ya Ghadir Khum baada ya kutawazwa Imam Ali, ikawa ni rahisi kwao kuigeuzia kuwa siku ya Arafah. Siku ya Ghadir ilikusanya jumla ya watu laki moja au zaidi na hakuna tukio munasaba katika Hijja ya kuaga linalofanana na Ghadir katika kulinganisha kuliko siku ya Arafa, kwani Mahujaji hawakukusanyika mahala pamoja isipokuwa sehemu mbili hizo, na kinachofahamika ni kuwa watu huwa wametawanyika kwa makundi mbali mbali katika siku zote za Hijja na wala hawakusanyiki mahala pamoja isipokuwa Arafa.


Kwa hiyo basi tunaona kwamba wale wasemao kuwa ilishuka siku ya Arafa wanasema kuwa iliteremka mara tu baada ya hotuba mashuhuri ya Mtume (s.a.w.) hotuba ambayo wameithibitisha wana hadithi ndani ya vitabu vyao. Basi iwapo tamko la Ukhalifa wa Ali bin Abi Talib wameliondosha kwenye ukweli wake na wakashitukiza watu miongoni mwao akiwa Ali mwenyewe na wale waliokuwa pamoja naye wakishughulika kuandaa mazishi ya Mtume kwa kumpa baia Abubakar huko kwenye Saqifah bani Saidah (Klabu ya Bani Saidah) bila kutegemea, na kisha wakayatupilia mbali yale maagizo ya Ghadir na kuyasahau kabisa, je,itawezekana kwa mtu yeyote baada ya hayo yaliyotokea kutoa hoja kuwa aya hiyo ilishuka siku ya Ghadir? Aya haiko wazi zaidi katika kufahamika maana yake kuliko hadithi ielezayo khabari ya Wilaya,(utawala) bali maana iliyo katika aya hiyo ni kukamilika kwa dini na kutimia kwa neema na kuridhika kwa Mola. Na hii si kwa kitu kingine ila ni ishara ya aya juu ya kupatikana kwa tukio katika siku hiyo nalo ndiyo sababu ya ukamilikaji wa dini.


Kinachotuongezea yakini juu ya kusihi kwa itikadi hii, ni ile khabari aliyoisimulia ibn Jarir kutoka kwa Qabaisah bin Abi Dhubaib amesema: "Kaabu alisema Lau wasiokuwa umma huu ndiyo ambao wangeshukiwa na aya hii basi wangeithamini siku iliyoshushwa ndani yake na wangeifanya kuwa ni sikukuu wanayokusanyika ndani yake", Umar akasema aya gani hiyo ewe Kaab" akasema: "Leo nimekukamilishieni dini yenu" Umar akasema, Hakika mimi nafahamu siku iliyoshuka na mahala ambapo ilishukia, ilishuka siku ya Ijumaa na ilikuwa siku ya Arafah na zote hizo Al-Hamdulillah kwetu sisi ni siku kuu".

Pili: Kauli isemayo kuwa aya ya "Leo nimekukamilishieni Dini yenu" kuwa ilishuka siku ya Arafah inapingana na aya ya "Tabligh" isemayo kuwa "Ewe Mtume fikisha yale uliyoteremshiwa" aya ambayo inamuamuru Mtume (s.a.w.) kufikisha jambo muhimu ambalo Utume hautimii ila kwa jambo hilo, na ni aya ambayo hapo kabla tumetangulia kuifanyia uchambuzi na ikabainika kuwa ilishuka baina ya Maka na Madina baada ya Hijja ya kuaga, khabari ambayo wameisimulia zaidi ya Masahaba mia moja ishirini na pia wameisimulia zaidi ya wanachuoni mia tatu na sitini wa Kisunni, basi ni vipi Mwenyezi Mungu ataikamilisha dini na kuitimiza neema yake siku ya Arafa kisha baada ya wiki moja amuamuru Mtume wake (s.a'.w.) wakati akirudi awafikishie watu jambo muhimu ambalo Utume wake hautakamilika isipokuwa kwa jambo hilo?
Vipi basi itasihi hali hiyo enyi wenye kutumia akili?


Tatu: Mwenye kuchunguza kwa undani atakapoifanyia mazingatio hotuba ya Mtume (s.a.w.) katika siku ya Arafah hawezi kukuta ndani ya hotuba hiyo jambo jipya ambalo Waislamu walikuwa hawalijuwi, kiasi ambacho iwezekane kuzingatiwa kuwa ni jambo muhimu ambalo kwalo Mwenyezi Mungu ameikamilisha dini na kuitimiza. Ndani ya hotuba hiyo hapakuwa isipokuwa ni mkusanyiko wa mausio ambayo Qur'an imekwisha kuyataja au mwenyewe Mtume alikwisha kuyaeleza ndani ya minasaba mingi tu na siku hiyo ya Arafah akawa anayasisitiza.
Hebu yaangalie mambo yaliyomo katika hotuba hiyo kama walivyoisajili wapokezi wote: Mwenyezi Mungu amezipa heshima damu zetu na mali zetu kama alivyoupa heshima mwezi wenu huu na siku yenu hii (kwa kuharamisha umwagaji damu katika mwezi huu). Mcheni Mwenyezi Mungu wala musiwapunje watu vitu vyao na wala musieneze ufisadi katika nchi, mwenye kuwa na amana na aitekeleze.

Watu wote ndani ya Uislamu wako sawa Mwarabu hana ubora juu ya asiyekuwa Mwarabu isipokuwa kwa kumcha Mungu. Kila damu iliyokuwa zama za jahiliya iko chini ya unyayo wangu (kuuawa mtu kwa kulipiza kisasi kwa mtindo wa zama za ujinga sasa hapana tena). Kila riba iliyokuwa katika zama za Jahiliyah iko chini ya unyayo wangu (yaani sasa hapana tena riba katika mfumo wa Jahiliyah, kabla ya kuja Uislam). Bila shaka idadi ya miezi mbele ya Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na miwili, kati ya hiyo iko minne ni mitukufu. Nakuusiyeni juu ya wanawake watendeeni wema, bila shaka ninyi mumewachukuwa chini ya amana ya Mwenyezi Mungu na mumezihalalisha tupu zao kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu.


Nakuusieni wale ambao imewamiliki mikono yenu ya kuume, walisheni kile mnachokula na muwavalishe kile munachovaa. Hakika Muslimu nduguye ni Muislamu, asimdanganye wala asimfanyie khiyana, wala usimsengenye wala damu yake si halali kwake wala chochote katika mali yake. Bila shaka shetani amekwisha kata tamaa ya kuabudiwa baada ya leo, lakini atatiiwa katika lisilokuwa hilo miongoni mwa matendo yenu mnayoyadharau. Adui mkubwa kwa Mwenyezi Mungu ni yule amuuwaye mtu ambaye Mwenyezi Mungu hataki kumuuwa na yule ampigaye asiyempiga, na mwenye kukufuru neema ya walii wake basi atakuwa amekufuru yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu kwa Muhammad, mwenye kujinasibisha kwa asiyekuwa baba yake basi laana ya Mwenyezi Mungu na Malaika wake na watu wote imshukie.


Hakika nimeamuriwa nipigane na watu mpaka waseme "Hapana mwenye haki ya kuabudiwa ila Mwenyezi Mungu na kwamba mimi ni Mtume wake", na wataposema hivyo, basi damu yao na mali zao zimehifadhika tokana nami isipokuwa kwa haki na hesabu yao iko kwa Mwenyezi Mungu. Msirudi ukafirini baada yangu mkawa wenye kupotea na kuuwana ninyi kwa ninyi. Haya yote ndiyo yaliyosemwa katika khutba ya Arafa kwenye Hija ya kuaga, nami nimekusanya milango yake kutoka kwenye rejea zote zinazotegemewa ili pasije bakia chochote miongoni mwa usia wa Mtume (s.a.w.) walioutaja wanachuoni wa hadithi isipokuwa niwe nimeutoa.
Basi je, ndani ya usia huo kuna jambo jipya kwa upande wa Masahaba?
Hapana kabisa, yote yaliyokuja ndani yake yametajwa ndani ya Qur'an na hukmu yake imebainishwa ndani ya Sunna ya Mtume, kwani Mtume (s.a.w.) alitumia uhai wake wote akiwabainishia watu yale waliyoteremshiwa na akiwafundisha yote madogo na makubwa, basi hakuna uhusiano wowote kwa kushuka aya ya kukamilisha dini na kutimiza neema na radhi ya Mwenyezi Mungu. Baada ya usia huu ambao Waislamu wanaufahamu, Mtume aliukariri kwao ili kutia mkazo kwani hiyo ilikuwa ni mara yao ya kwanza kukusanyika mbele ya Mtume kwa idadi hiyo kubwa, na pia kabla ya kutoka kwenda Hijja Mtume aliwaambia kuwa hiyo ni Hijja yake ya kuaga, kwa hiyo basi ilikuwa ni wajibu kwake kuwasikilizisha usia huo.


Ama kama tutaichukua ile kauli ya pili, nayo ni ile ya kushuka kwa aya hiyo siku ya Ghadir Khum baada ya kusimikwa Imam Ali kuwa ni khalifa wa Mtume (s.a.w.) na ni amiri wa Waumini, hapana shaka ile maana inalingana na kuafiki, kwani Ukhalifa baada ya Mtume (s.a.w.) ni miongoni mwa mambo muhimu na wala Mwenyezi Mungu hawezi kuwaacha waja wake hivi hivi tu, wala haipasi kwa Mtume kuondoka tu bila ya kuweka kiongozi na kuuacha umma wake bila mchungaji, na hali ya kuwa yeye Mtume alikuwa haondoki Madina ila atamwacha mtu miongoni mwa Masahaba kuwa Khalifa wake hapo mjini, basi ni vipi tutaamini kuwa alifariki na hakufikiria juu ya suala la Ukhalifa?


Iwapo wasiokuwa na dini katika zama zetu hizi wanauamini msingi huu (wa kuacha mtu maalum baada ya mtawala kuondoka) na hufanya kila njia kumbainisha mrithi wa Rais hata kabla ya Rais huyo kufariki ili tu waweze kuwaongoza watu wasiwaache hata siku moja bila ya kuwa na Rais!! Basi haiwezekani kabisa kuwa dini ya Kiislamu ambayo ni dini iliyokamilika kuliko zote na imetimia, na ni dini ambayo Mwenyezi Mungu alihitimisha kwayo sheria zote, haiwezekani kamwe kulipuuza jambo muhimu kama hili. Na hapo kabla tumefahamu kwamba bibi Aisha na ibn Umar na kabla yao Abubakr na Umar kila mmoja wao alitambua kwamba hapana budi Khalifa abainishwe vinginevyo basi itatokea fitna, kama ambavyo jambo hilo walilitambua pia wale waliokuja baada yao miongoni mwa Makhalifa ndipo kila mmoja wao alimbainisha atakayekuja baada yake, basi ni vipi hekima hii inapotea kwa Mwenyezi Mngu na Mtume wake?


Basi kauli isemayo kuwa Mwenyezi Mungu alimpelekea Wahyi Mtume wake katika ile aya ya mwanzo "Aya ya Tabligh, kufikisha" wakati akirejea toka kwenye Hijja ya kuaga kwamba amsimike Ali kuwa Khalifa wake pale Mwenyezi Mungu aliposema: "Ewe Mtume fikisha yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako na kama hukufanya, basi hujafikisha ujumbe wake na Mwenyezi Mungu atakulinda kutokana na watu". Hii ikiwa na maana kwamba: Ewe Muhammad iwapo hautafikisha nililokuamuru ya kwamba Ali ndiye msimamizi wa waumini baada yako basi ni kama kwamba hukukamilisha umuhimu wa jambo ambalo kwalo umetumwa, kwani kukamilika dini kwa Uimamu ni jambo la lazima kwa kila wenye akili.


Na inaonesha kwamba Mtume (s.a.w.) alikuwa akichelea upinzani wao kwake na kumkadhibisha, kwani imekuja ndani ya baadhi ya riwaya kauli ya Mtume (s.a.w.) isemayo: "Kwa hakika Jibril ameniamuru kutoka kwa Mola wangu kwamba nisimame mahala hapa na nimjulishe kila aliye mweupe na mweusi yakuwa Ali bin Abi Talib ni ndugu yangu na ni wasii wangu na ni Khalifa wangu na ni Imam baada yangu, nikamuomba Jibril anitakie msamaha kwa Mola wangu (juu ya jambo hili) kutokana na kutambua kwangu uchache wa wamchao Mungu (miongoni mwa sahaba zangu) na kuwepo wengi wanao nibughudhi kwa ajili ya mimi kushikamana mno na Ali na kumuelekea mno yeye Ali mpaka wakaniita kuwa (Udhunu) mtu asikilizaye kila aambiwalo kwa kauli moja. Na kwa hilo Mwenyezi Mungu akasema: "Na miongoni mwao wako ambao wanambughudhi Mtume na wanamuambia kuwa yeye huamini kila aambiwalo" lau ningetaka kuwataja na kuwatambulisha ningefanya hivyo lakini nimewaheshimu kwa kuwasitiri, basi Mwenyezi Mungu hakuridhia isipokuwa kufikisha (aliyoniamuru) kuhusu Ali, fahamuni enyi watu ya kwamba Mwenyezi Mungu amekuchagulieni Ali awe ni mtawala na kiongozi na amefaradhisha kwa kila mtu amtii...[40]


Mwenyezi Mungu alipomteremshia Mtume (s.a.w.) kauli yake isemayo: "Na Mwenyezi Mungu atakulinda kutokana na watu." Pale pale bila kuchelewa Mtume alitekeleza amri ya Mola wake akamtawalisha Ali kuwa ni Khalifa baada yake na akawaamuru Masahaba wake kumpongeza kwa uamiri wake kwa waumini na wakampongeza, na baada ya hapo ndipo Mwenyezi Mungu alipowateremshia kauli yake isemayo: -
"Leo nimekukamilishieni Dini yenu na nimeitimiza neema yangu kwenu na nimewaridhia Uislamu kuwa ndiyo dini yenu". Zaidi ya yote hayo ni kwamba sisi tunawakuta baadhi ya wanachuoni wa Kisunni wanakiri wazi wazi kuwa aya ya Tablighi ilishuka kuhusu Uimamu wa Ali, wamepokea kutoka kwa Ibn Mar-Dawaih naye toka kwa ibn Mas-ud amesema: "Katika zama za Mtume tulikuwa tukisoma, Ewe Mtume fikisha uliyoteremshiwa toka kwa Mola wako- kwamba Ali ni mtawala wa kila muumini - na ikiwa hutafanya, basi hujafikisha ujumbe wake na Mwenyezi Mungu atakulinda kutokana na watu". Na baada ya uchunguzi huu tukiongezea riwaya za Kishia zitokazo kwa Maimamu watakatifu inatubainikia kwamba Mwenyezi Mungu aliikamilisha dini yake kwa Uimamu, na kwa ajili hiyo basi Uimamu kwa Mashia umekuwa ni msingi miongoni mwa misingi ya dini.


Na kwa Uimamu wa Ali bin Abi Talib Mwenyezi Mungu alitimiza neema yake kwa Waislamu ili wasije baki hivi hivi tu wakivutwa na matamanio na fitna ikiwatenganisha na watawanyike kama kondoo wasio na mchungaji. Mwenyezi Mungu aliwaridhia Uislamu kuwa ndiyo dini yao kwani yeye Mwenyezi Mungu aliwachagulia Maimamu aliowaondolea uchafu na kuwatakasa kisha akawapa hekima na kuwarithisha Elimu ya Kitabu ili wawe ni mawasii wa Muhammad (s.a.w.) hivyo basi ni wajibu juu ya Waislamu wayaridhie maamuzi ya Mwenyezi Mungu na wakubaliane na uchaguzi wake kikamilifu, kwani Maf-humu ya Uislamu kwa ujumla ni kusalimu amri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amesema:
"Na Mola wako ndiye anayeumba akitakacho na ndiye anayechagua (akitakacho) wao hawana uchaguzi (hiyari) ametakasika Mwenyezi Mungu na ametukuka kutokana na vile wanavyomshirikisha, na Mola wako anajua yanayofichwa na nyoyo zao na yale wanayoyadhihirisha naye Mwenyezi Mungu (ni yeye tu peke yake) hapana Mola ila yeye, ni zake sifa zote njema mwanzoni na mwishoni na hukmu pia ni yake na kwake ndiko mtarejeshwa" (Qur'an, 28:68-70)


Na kwa kupitia yote hayo inafahamika kwamba siku ya Ghadir Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) aliifanya kuwa ni siku ya Sikukuu kwani baada ya kumtawalisha Imam Ali na baada ya kumshukia kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Leo nimekukamilishieni Dini yenu..." Mtume alisema: Ashukuriwe Mwenyezi Mungu kwa kuikamilisha dini na kuitimiza neema na Mola ameuridhia Utume wangu na utawala wa Ali bin Abi Talib baada yangu[41] kisha akamtengenezea jukwaa ili Waislamu wampongeze, na Mtume alikaa ndani ya hema na akamkalisha Ali pembeni yake kisha akawaamuru Waislamu wakiwemo wakeze Mtume waingie kwa makundi makundi wampongeze Ali kwa cheo hicho na wamsalimie kwa maamkizi ya kuwa kwake Amirul-Muuminina.watu wakafanya walichoamuriwa, na miongoni mwa waliompongeza Amirul-Muuminina Ali bin Abi Talib katika tukio hili ni Abubakar na Umar.


Walimjia wawili hawa (Abubakar na Umar) wakamwambia hongera hongera ewe Mwana wa Abu Talib umepambazukiwa na kumekuchwea hali ya kuwa ni mtawala wetu na ni mtawala wa kila muumini mwanamume na mwanamke.[42] Na pindi Has-san bin Thabit aliyekuwa mshairi wa Mtume (s.a.w.) alipotambua furaha ya Mtume kuhusiana na siku hiyo alisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu unaniruhusu niseme beti za shairi utazozisikiliza kuhusiana na mahala hapa." Mtume akasema, "Kwa baraka za Mwenyezi Mungu sema, (ewe) Has-san hukuacha kuwa ni mwenye kuungwa mkono na roho tukufu muda wote unapotunusuru kwa ulimi wako". Basi akasoma ushairi ufuatao: "Siku ya Ghadir Mtume wao anawaita hapo Khum, Hebu sikiliza Mtume anatangaza..." Mpaka mwisho wa beti ambazo wamezitaja wanahistoria.[43]


Lakini pamoja na yote hayo. hakika Maquraishi walijichagulia wenyewe (Kiongozi wao) na wakapinga Utume na Ukhalifa kuwa kwa bani Hashim wasije jifakharisha mno kwa watu wao, hayo ni kama alivyobainisha Umar bin Al-Khattab kwa Abdallah bin Abbas katika mazungumzo yaliyofanyika baina yao:[44] Taz: Tarikhut-Tabari Juz. 5 uk. 31, Tarikhu Ibnul-Athir Juz. 3 uk. 31 na Shark Nahjul-Balagha ya Ibn Abil-Hadi Juz. 2 uk. 18. Basi hapakuwa na yeyote aliyesherehekea sikukuu hiyo baada ya kutajwa kwake kwa mara ile ya kwanza ambayo Mtume alisherehekea. Na iwapo kama walijisahaulisha tamko la Ukhalifa (alilolitamka Mtume) na wakalififisha akilini mwao na haukupita muda isipokuwa miezi miwili (tangu kutamkwa) pamoja na muda huo (mchache) hapana yeyote aliyezungumzia, ni vipi kumbukumbu ya Ghadir itakumbukwa baada ya kupita mwaka kamili?


Na ilipita miaka mingi mpaka pale haki iliporejea kwa mwenye nayo baada ya robo karne, hapo ndipo Imam Ali akaifufua upya siku hiyo baada ya kuwa ilikuwa karibu kuzikwa, hapa ilikuwa katika ukumbi wa Msikiti wa Al-Kuufah Iraq, wakati Imam Ali alipowataka Masahaba wa Muhammad (s.a.w.) wakiwemo wale waliohudhuria sikukuu ya Ghadir wasimame na washuhudie mbele ya watu baia ya Ukhalifa (iliyofanyika siku hiyo) wakasimama Masahaba thelathini, kumi na sita miongoni mwao walikuwa ni mashujaa wa Badri (wote) wakashuhudia.[45] Ama yule aliyeficha ushahidi huo na kudai kuwa amesahau kama alivyofanya Anas bin Malik ambaye ilimsibu dua ya mja mwema kwani hakuwahi kusimama toka mahala alipokuwa ila alipatwa na maradhi ya mbaranga, basi akawa siku zote hulia na kusema, yamenisibu maombi ya mja mwema kwani nilificha ushahidi wake.[46] Kwa tendo hilo (la ushahidi) Abul-Hasan aliisimamisha hoja juu ya umma huu, na tangu zama hizo mpaka leo hii na mpaka Qiyama Mashia wanasherehekea kumbukumbu ya siku ya Ghadir na kwao ni sikukuu kubwa. Ni kwanini isiwe hivyo hali ya kuwa ndiyo siku ambayo Mwenyezi Mungu alitukamilishia dini na akatutimizia neema yake na kuturidhia Uislamu kuwa ndiyo dini yetu, nayo ni siku yenye utukufu mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake na waumini.


Baadhi ya wanachuoni wa Kisunni wameeleza toka kwa Abu Huraira kwamba amesema: "Pindi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alipoushika mkono wa Ali na akasema, yeyote ambaye mimi nilikuwa mtawalia mambo yake basi Ali ni mtawalia mambo yake... mpaka mwisho wa khutba Mwenyezi Mungu aliiteremsha "Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimeitimiza neema yangu kwenu na nimewaridhia Uislamu kuwa ndiyo dini yenu". Abu Huraira amesema: "Ilikuwa ni siku ya Ghadir Khum, basi yeyote mwenye kufunga siku ya kumi na nane mfunguo tatu huandikiwa thawabu za miezi sitini". Taz: Al-Bidaya Wan-Nihayah, Juz. 5 uk. 214.


Ama riwaya za Mashia kutoka kwa Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) zinazohusu ubora wa siku hiyo ni nyingi mno, basi kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu aliyetujaalia kuwa miongoni mwa wanaoshikamana na utawala wa Amirul-Muuminina Ali (a.s.) na wenye kusherehekea sikukuu ya Ghadir. Kwa kufupisha uchambuzi huu ni kwamba hadithi ya Ghadir isemayo; "Yeyote ambaye mimi nilikuwa natawalia mambo yake basi huyu Ali ni mtawalia mambo yake, ewe Mwenyezi Mungu muunge atakayemuunga, na umpinge atakayempinga, na umsaidie atakayemsaidia na umdhalilishe atakayemdhalilisha na izungushe haki anako zungukia". Hadithi hii au bora ni zaidi kusema, "Ni tukio kubwa la kihistoria ambalo umma wa Kiislamu umeafikia na katika kulinakili, na hapo kabla tumetajiwa wanachuoni mia tatu na sitini wa Kisunni na wengine wa Kishia zaidi ya hao wa Kisunni".


Na yeyote atakaye kutafiti na kupata ziyada, basi ni juu yake kuangalia Kitabul-Ghadir cha Al-Allamah Al-Amin. Baada ya haya tuliyoyaeleza basi siyo ajabu umma wa Kiislamu kugawanyika Masunni na Mashia.Kundi la kwanza limeshika maana na misingi ya Shuraa,yaani mashauriano yaliyofanyika katika klabu ya Bani Saidah, na kuyabadilisha matamko ya wazi (aloyatoa Mtume) na hivyo kwenda kinyume na kile ambacho wapokezi wa hadithi ya Ghadi wameafikiana pia maelekezo mengine (ya Mwenyezi na Mtume). Kundi la pili halikubali badali na limewapa baia Maimamu kumi na wawili kutoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.) na halikutaka kinyume chao. Ukweli halisi ulivyo ni kwamba, mimi kila ninapoyachunguza Madhehebu ya Kisunni hasa juu ya hili suala la Ukhalifa ninakuta limejengeka kwenye msingi wa dhana na Ij-Tihadi, kwani kanuni ya uchaguzi haina dalili madhubuti ndani yake na hiyo ni kwa kuwa yule mtu tunayemchagua leo hii (tunamuona) ni bora kuliko mwingine na hali sisi hatujui khiyana ya macho na yaliyofichwa nyoyoni, na kwa kuwa sisi wanaadamu ukweli ulivyo tumeumbwa na sifa ya upendeleo chuki na ubinafsi uliomo ndani ya nafsi zetu na umbile hili linaweza kuitumia nafasi yake ikiwa suala la kumchagua mtu litawakilishwa kwetu.


Na mas'ala niliyoyatoa siyo jambo la kubuni au la kutia chumvi, kwani yeyote atakayeifuatilia fikra hii, yaani fikra ya (watu) kumchagua Khalifa atakuta kwamba msingi huo unaopigiwa ngoma haukufanikiwa na kamwe hauwezi kufanikiwa. Huyu hapa Abubakr ambaye ndiye kiongozi wa hiyo Shuraa, pamoja na kuwa yeye aliupata Ukhalifa kwa uchaguzi wa kushauriana, tunamuona yeye wakati alipokaribia kufariki haraka sana alimteuwa Umar bin Al-Khatab awe Khalifa wake bila ya kutuma njia ya mashauriano.

Na Umar bin Al-Khatab ambaye alishiriki kuujenga Ukhalifa wa Abubakr tunamuona baada ya kufariki Abubakr anawatangazia waislamu kwamba, "Baia ya Abubakar ilikuwa ni jambo lililopatikana ghafla Mwenyezi Mungu aliwakinga Waislamu kutokana na shari yake".[47]
Kisha baada ya hayo tunamuona Umar wakati aliposhambuliwa na akayakinisha kwamba ajali yake imekaribia alichagua watu sita ili wamchague mmoja miongoni mwao awe Khalifa na hali ya kuwa anafahamu fika kwamba kikundi hiki pamoja na uchache wao watahitilafiana licha ya kuwa wao ni masahaba wa mwanzo kuingia katika Uislamu na ni wachamungu, bila shaka upendeleo wa kibinaadamu utajitokeza, hataepukana nao isipokuwa yule aliye Maasum, na kwa ajili hiyo tunamuona eti kwa kuzuwia hitilafu anaupa uzito upande wa Abdur-Rahman bin Auf akasema: "Iwapo mtahitilafiana basi kuweni upande ule alioko Abdur-Rahman". na baada ya hapo wakamchagua Imam Ali ili awe Khalifa lakini wakamuwekea sharti kuwa awahukumu kwa mujibu wa kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake na Sunna ya Masheikh wawili yaani Abubakar na Umar.


Imam Ali alikubali kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wa Mungu na alikataa kuhukumu kwa mujibu wa Sunna ya Masheikh wawili.[48] Ama Uthman yeye alilikubali sharti hili nao wakampa baia ya Ukhalifa na ndipo Imam Ali aliposema: "Oh! haulingani ukhalifa wa Mwenyezi Mungu na Shuraa! ni lini imeingia shaka kati yangu na Khalifa wa kwanza miongoni mwao, mpaka imefikia nilinganishwe na watu kama hawa lakini mimi nilikwenda nao kama walivyokwenda, bali kuna mtu miongoni mwao ameelemea kwenye chuki zake, na mwingine kuelemea kwenye ujamaa wake".[49]
Ikiwa hawa ndiyo wateule miongoni mwa Waislam, na ni watu makh-susi kati ya watu wanaotegemewa,ni vipi upendeleo unawachezea na wanakuwa na chuki na ubinafsi kati yao?


Hali hii iko wazi kwani Abdur-Rahman bin Aufi hatimaye alijutia uchaguzi alioufanya, akamkasirikia Uthman na akamtuhumu kwa kwenda kinyume cha ahadi yalipotokea yaliyotokea, na Masahaba wakubwa wakamjia wakamwambia: "Ewe Abdur-Rahman hii ndiyo kazi iliyofanywa na mikono yako". Akawaambia: "Nilikuwa simdhanii kwa haya (ayatendayo) lakini namuapa Mwenyezi Mungu kwamba kamwe sitamsemesha". Kisha Abdur-Rahman bin Auf alifariki hali ya kuwa amemkasirikia Uthrnan, mpaka wamesimulia kwamba Uthman alikwenda kumzuru Abdur-Rahman alipokuwa mgonjwa basi Abdur-Rahman aligeuzia uso wake ukutani na hakumsemesha.[50]


Hatimaye yakawa yaliyokuwa, mapinduzi yakasimama na mwishoni mwake Uthman akauawa umma ukarejea tena baada ya hapo kwenye uchaguzi na safari hii wakamchagua Ali. Lakini waja wa Mwenyezi Mungu wana kila hali ya kusikitikiwa, kwani Dola ya Kiislamu ilikwisha vurugika ikawa ni uwanja wa wapinzani na wenye tamaa ya kukalia cheo cha Ukhalifa kwa thamani yeyote ile na kwa njia yeyote ile japokuwa kwa kuuwa watu wasio na makosa, hukmu za Mwenyezi Mungu na Mtume wake zikawa zimebadilishwa kwa muda huo wa miaka ishirini na mitano, hapo Imam Ali (a.s.) alijikuta yuko katikati ya bahari yenye mawimbi yanayopigana yenyewe kwa yenyewe tena kwenye kiza nene na upepo mkali.


Hivyo basi alimaliza Ukhalifa wake katika vita zilizomwaga damu, vita ambavyo vililazimishwa na wapinzani na waliotoka katika dini, na hakutoka kwenye vita isipokuwa kwa kuuawa kishahidi hali ya kuwa akiusikitikia umma wa Muhammad. Mwana wa muachwa huru Muawiyah bin Abisufiyan aliingiwa na tamaa ya Ukhalifa na walio kama yeye kama kina Amri bin-Al-as na Mughirah bin Shuubah na Mar-wan bin Al-Hakam na wengineo wengi, na hakuna kilichowafanya watu hawa wathubutu kufanya hayo waliyoyafanya isipokuwa ni ile fikra ya Shuraa na uchaguzi.

Umma wa Muhammad ukawa umezama ndani ya bahari ya damu na watu wapumbavu na watwevu ndio wakawa wanauamulia umma huu hatima yake na baadaye Shuraa ikageuka na kuwa Ufalme mfano wa utawala wa Kaisari na Kisra. Basi kipindi hicho kikapita, kipindi ambacho wamekipa jina la Ukhalifa uliyoongoka na kwa jina la Ukhalifa huo wakaitwa Makhalifa wanne kuwa ndiyo waongofu, lakini ukweli ulivyo ni kuwa hata hawa wanne hawakuwa Makhalifa kwa kuchaguliwa na kwa mashauriano isipokuwa Abubakar na Ali, na tukimtoa Abubakar kwani baia yake ilikuwa ya kushitukiza bila kutegemea kwa mujibu wa usemi wa Umar ambapo izingatiwe kuwa halikuhudhuria kwenye baia hiyo "Kundi la upinzani" kama isemwavyo leo hii nalo ni la Ali na Bani Hashim na wale wenye mtazamo kama wa Bani Hashim, hakuna anayebakia ambaye baia yake ilifungamana na njia ya mashauriano na uchaguzi isipokuwa Ali bin Abi Talib ambaye Waislamu walimbai atake asitake pamoja na hayo baadhi ya masahaba waligoma lakini Imam Ali hakuwalazimisha wala kuwatishia.


Mwenyezi Mungu alitaka Ali bin Abi Talib awe khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa tamko litokalo kwa Mwenyezi Mungu na kwa uchaguzi wa Waislamu, na umma wa Kiislamu wote Masunni na Mashia wamekubaliana juu ya ukhalifa wa Ali na wamehitilafiana juu ya ukhalifa wa wengine kama ambavyo jambo hili liko wazi. Mimi nasema; "Wanafaa kusikitikiwa waja (wa Mwenyezi Mungu) lau wao wangekubali alichowachagulia Mwenyezi Mungu basi wangeneemeka kila upande na Mwenyezi Mungu angewateremshia baraka nyingi kutoka mbinguni na leo hii Waislamu wangekuwa ndiyo mabwana wa ulimwengu na ni viongozi wake kama alivyowatakia Mwenyezi Mungu lau wangelimfuata" "Nanyi ni watukufu ikiwa ni wenye kuamini."


Lakini ibilisi aliyelaaniwa, adui yetu aliyedhahiri alisema kumwambia Mwenyezi Mungu: "Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi nitawakalia (waja wako) katika njia yako iliyonyooka (Ili niwapoteze) kisha nitawaijia kwa mbele yao na nyuma yao na kuliani kwao na kushotoni kwao na wengi katika wao hutawakuta wenye kukushukuru" (Qur'an, 7:16-17). Basi mwenye akili na aiangalie hali ya Waislamu katika ulimwengu, wao ni madhalili hawawezi chochote wanakimbia nyuma ya madola mengine na wanaitambua Israel wakati yenyewe inakataa kuwatambua na hata kidogo haiwaruhusu kuingia katika Qudsi ambayo sasa imekuwa ndiyo mji wake mkuu, na unapowaangalia Waislamu utawaona wako chini ya huruma ya Amerika na Urusi, na kwa kweli umasikini umeyatafuna mataifa yao na wanauawa kwa njaa na maradhi wakati mbwa wa Ulaya wanakula aina mbali mbali za nyama na samaki, "Lahaula wala Quwwata IllaBillah".

Bibi Fatma (a.s.) mbora wa wanawake alieleza wakati alipomgombeza Abubakr kisha akatowa hotuba kwa wanawake wa Muhajirina na Answari na mwisho wa hotuba hiyo alieleza habari ya hatima ya umma huu akasema, "Ama naapa hatua ya mwanzo imefanywa tungoje huenda ikaleta matunda wamefanya mambo yaliyoleta maangamizi, hapo watakuwa hasarani watenda batili na watajua watakaofuatia maovu yaliyowapata wa mwanzo, kisha furahieni dunia yenu na kuweni na yakini kuwa fitna ihangaishayo nyoyo itakuja, na tazamieni upanga mkali, na ukali wa muamizi dhalimu na vurugu itakayoenea kila mahali na ubinafsi wa wadhalimu utaacha hali yenu ya ulinzi dhalili na kuangamiza umoja wenu, hasara iliyoje kwenu!Mmekuwa hamtambui je tukulazimisheni kuyatambua hayo hali yakuwa hampendi?[51]

Alisema kweli mbora wa wanawake kwa aliyo yaeleza naye ni bintiye Mtume, Mtume ambaye ni chimbuko la ujumbe usemi wake bi Fatma umejaa maelezo kuhusu hali ya baadaye ya maisha ya umma huu toka pale umma ulipogeuka nyuma. Basi nani ajuaye huenda yanayotazamiwa kutokea ni mabaya mno kuliko yaliyopita, hayo ni kwa kuwa waliyachukia aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu wakaharibu mtendo yao.