ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

 

UFAFANUZI
Pamoja na kwamba Imam Muslim amelifupisha tukio hili na hakulisimulia kikamilifu, lakini Al-Hamdulillah inatosheleza na labda ufupisho huu ulitoka kwa Zaid bin Ar-Qam mwenyewe pale hali halisi ya kisiasa ilipomlazimisha kuificha hadithi ya Ghadir na hili tunalifahamu kutokana na mfumo wa hadithi ulivyokuja kwani msimuliaji anasema:

"Mimi, Husain bin Sabrah o na Umar bin Muslim tulikwenda kwa Zaid bin Ar-Qam, tulipokaa Husain akamwambia Zaid, Bila shaka ewe Zaid umepata kheri nyingi, umemuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) umesikia hadithi zake na umepigana vita pamoja naye na umesali nyuma yake, kwa hakika umepata kheri nyingi mno, hebu tusimulie ewe Zaidi yale uliyoyasikia kwa Mtume (s.a.w.)". Zaid akasema, "Ewe mtoto wa ndugu yangu nimekwisha kuwa mzee sasa na umekuwa mrefu muda wangu, nimesahau baadhi ya mambo ambayo nilikuwa nikiyahifadhi toka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) basi yale nitakayokusimulieni yakubalini na yale nisiyokusimulieni msinilazimishe, kisha akasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu siku moja alisimama kwenye maji yaitwayo Khum akahutubia..."


Kutokana na mtiririko wa hadithi inadhihiri kwamba, Husain alimuuliza Zaid bin Ar-Qam tukio la Ghadir naye Zayd akalitoa jibu la suali hili mbele ya wote waliohudhuria, hivyo basi hapana shaka Zaid alikuwa akitambua kwamba kutoa jawabu la wazi wazi juu ya suali hilo ingemsababishia matatizo mbele ya serikali ambayo ilikuwa ikiwalazimisha watu kumlaani Ali bin Abi Talib, na kwa ajili hii tunamkuta anajitetea kwa muulizaji ya kuwa sasa amekuwa mtu mzima na muda mrefu umempitia na ameyasahau baadhi ya mambo aliyokuwa akiyahifadhi, kisha anaongeza kwa kuwataka waliohudhuria wakubali yale anayowasimulia na wala wasimlazimishe kuyasimulia yale anayotaka kuyanyamazia.

Pamoja na woga wake na kulifupisha kwake tukio hili bila shaka Zaidi bin Ar-Qam (Mwenyezi Mungu amlipe Kheri) ameubainisha ukweli mwingi na akaichenga hadithi ya Ghadir hakuitaja ile kauli yake isemayo "Mtume (s.a.w.) alisimama akatuhutubia kwenye bonde la Khum liliko kati ya Maka na Madina," kisha baada ya hapo akataja ubora wa Ali (a.s.) na kwamba yeye ni mshirika wa Qur'ani katika hadithi ya vizito viwili, kitabu cha Mwenyezi Mungu na watu wa nyumba yangu", na hakulitaja jina la Ali (a.s.) akawaachia waliohudhuria hapo hapo watumie akili zao kwani Waislamu wote wanafahamu kwamba Ali(a.s.) ndiyo kiongozi wa watu wa nyumba ya Mtume.


Na ndiyo maana tunamuona hata Imam Muslim mwenyewe alifahamu kutokana na hadithi hiyo kile ambacho sisi tumekifahamu, kwani ameiandika hadithi hii katika mlango wa Fadhail za Ali bin Abi Talib(a.s.) ingawaje hadithi haikutaja jina la Ali bin Abi Talib!! Taz: Sahih Muslim Juz. 7 uk. 122 Babu Fadhail Ali. 5) At-Tabrani amethibitisha ndani ya Muujamul-Kabir kwa sanad iliyo sahihi toka kwa Zaid bin Ar-Qam na Hudhaifah bin Usayd Al-Ghifari amesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu alihutubia huko Ghadir Khum chini ya miti akasema:

"Enyi watu yakaribia nitaitwa na nitaitika, nami nitaulizwa nanyi mtaulizwa, ni nini mtakachokisema?" Wakasema, "Tunashuhudia ya kwamba wewe umefikisha na umepigania (dini) na umetoa nasaha Mwenyezi Mungu akulipe mema". Mtume akasema, "Je, hivi hamushuhudii ya kwamba hapana Mola wa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wake, na kwamba pepo yake ni kitu cha kweli na moto wake ni kitu cha kweli, na kuwa mauti ni kitu cha kweli na kwamba kufufuliwa baada ya kufa ni kitu cha kweli. Na kwamba kiyama kitakuja bila ya shaka yoyote na kwamba Mwenyezi Mungu atawafufua waliomo makaburini?

Wakasema, tunashuhudia yote hayo," Mtume akasema: "Ewe Mwenyezi Mungu shuhudia" kisha akasema, "Enyi watu hakika Mwenyezi Mungu ni mtawalia mambo yangu na ni mtawalia mambo ya waumini nami ni bora mno kuliko nafsi zao, basi yeyote ambaye mimi ni mtawalia mambo yake huyu hapa ni mtawala wake (yaani Ali.) ewe Mwenyezi Mungu msaidiye atakayemsaidia na umfanye adui atakayemfanya adui kisha akasema, "Enyi watu hakika mimi nakutangulieni nanyi mutanifikia kwenye haudh, haudh ambalo upana wake ni kati ya Basra na San-aa, kwa hakika nitakuulizeni mtaponifikia kuhusu vizito viwili ni vipi mtanifuata katika vizito hivyo, kizito kikubwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu sehemu ya ncha yake iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu na nyingine iko mikononi mwenu, shikamaneni nayo msipotee wala msibadilishe, na (kizito cha pili) ni kizazi changu watu wa nyumba yangu, hapana shaka Mwenyezi Mungu mjuzi amenijulisha mimi ya kwamba viwili hivi havitatengana mpaka vinifikie kwenye Haudh."


Taz: Ibn Hajar ndani ya Sawaiq uk. 25 amenakili kwa Tabrani, Al-Hakim na Tir-midhi. 6) Kama ambavyo amethibitisha Imam Ahmad kwa njia ya Al-Barraa bin Azib kwa njia mbili amesema: "Tulikuwa pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu tukafika Ghadir-Khum, ikanadiwa sala ya jamaa Mtume akaandaliwa mahali chini ya miti miwili akaswali sala ya adhuhuri na akaushika mkono wa Ali kisha akasema: "Je, hamjui kwamba mimi ni bora mno kwa waumini kuliko nafsi zao" Wakasema kwa nini (twalijua hilo), akaushika mkono wa Ali(a.s.) kisha akasema, yeyote ambaye mimi ni mtawala wa mambo yake basi Ali ni mtawala wa mambo yake, Ewe Mwenyezi Mungu msaidie atakaye msaidia na mfanye adui atakayemfanyia uadui." Baada ya tukio hilo Umar akamkuta Ali akamwambia, "Hongera Ewe mwana wa Abu Talib umekuwa mtawalia mambo ya kila muumini mwanaume na mwanamke". Taz: Musnad Ahmad bin Hanbal Juz. 4 uk. 281 Kanzul-Ummal Juz. 15uk. 117. Fadhailul-Khamsah Minas-Sihahis-Sittah. Juz. 1 uk. 350.


Na kwa kifupi hadithi ya Ghadir (wameisimulia) wanachuoni wengi wa Kisunni zaidi kuliko tuliowataja, k.m Tirmidhi, Ibn Asakir, Abunuaim, Ibnul-Athir, Al-Khawar-Zami na Suyuti. Wengine ni Ibn Al-Haithami, Ibnus-Sabbagh Al-Maliki, Al-Al-Hanafi, Ibnul-Maghazili, Al-Humuwaini, Al-Haskani, Al-Ghazali na Bukhari ndani ya tarikh yake. Al-Allamah Al-Amin mwenye kitabu cha Al-Ghadir amewataja wanachuoni wa Kisunni walioisimulia hadithi hii ya Ghadir na wakaithibitisha ndani ya vitabu vyao, pamoja na tofauti zao za kimadhehebu tangu karne ya kwanza Hijiriyyah mpaka karne ya kumi na nne. Idadi yao ilikuwa inazidi wanachuoni mia tatu na sitini, na yeyote mwenye kutaka ushahidi basi ni juu yake kukirejea kitabu cha Al-Ghadir.[35]

Basi Je baada ya yote haya inawezekana akasema mwenye kusema kwamba hadithi ya Ghadir ni miongoni mwa uzushi wa Kishia?
Kinachoshangaza ni kuwa, wengi wa Waislamu wakati unapowatajia hadithi ya Ghadir hawaifahamu au unaweza kusema kuwa hawajaisikia.La kushangaza zaidi kuliko hili ni kwamba, ni vipi basi wanachuoni wa Kisunni baada ya kuwepo kwa hadithi hii ambayo imekubaliwa usahihi wake wanadai kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuacha Khalifa (aliyembainisha) bali aliacha jambo hili liwe la mashauriano miongoni mwa Waislamu?


Basi je, kuna hadithi iliyotoa maana ya wazi kuhusu Ukhalifa na ikabainisha kuliko hii enyi waja wa Mungu? Kwa hakika mimi nayakumbuka majadiliano yangu na mmoja wa wanachuoni kutoka Az-Zaitunah nchini kwetu pale nilipomtajia hadithi ya Ghadir nikiitolea ushahidi juu ya Ukhalifa wa Ali (a.s.), basi alikiri kuwa hadithi hiyo ni sahihi bali aliiongezea nguvu akanionyesha tafsiri ya Qur'an aliyoiandika yeye mwenyewe, tafsiri ambayo ndani yake ameitaja hadithi ya Ghadir na kuwa ni sahihi na baada ya hapo akasema ndani ya tafsiri yake:

"Mashia wanadai kwamba hadithi hii ni tamko linalohusu Ukhalifa wa Ali Karrama Llahu Waj-hahu na madai hayo ni batili kwa Masunni kwani yanapingana na ukhalifa wa bwana wetu Abubakar As-Siddiq na bwana wetu Umar Al-Faruq na bwana wetu Uthman Dhin-Nurain, basi hapana budi kulipa tafsiri nyingine tamko la Al-Maula (mtawalia mambo) lililokuja ndani ya hadithi hii liwe na maana ya mpenzi na msaidizi kama ilivyokuja ndani ya Qur'an na hivi ndivyo walivyolifahamu Makhalifa waongozi na Masahaba watukufu Mwenyezi Mungu awawie radhi wote, na hivi ndivyo walivyochukua toka kwao waliofuatia na wanachuoni wa Kiislamu. Basi hapana mazingatio yoyote kwa tafsiri ya Marafidhi (Mashia) kuhusu hadithi hii kwani wao hawakubali ukhalifa wa makhalifa (Abubakar, Umar, Uthman) na wanawatukana Masahaba wa Mtume na hili peke yake linatosha kuupinga uzushi wao na kuyabatilisha madai yao" Mwisho wa maneno yake yaliyomo ndani ya kitabu chake.


Basi mimi nilimuuliza: "Je, tukio hili lilitokea huko Ghadir Khum?"
Akajibu "Lau lingekuwa halikutokea wanachuoni na wataalam wa hadithi wasingelisimulia"!! Nikasema:
"Hivi kweli inakubalika kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) kuwakusanya Masahaba wake katika jua kali linalounguza na kuwahutubia hotuba ndefu ili tu awaambie kuwa Ali ni mpenzi wenu na mtetezi wenu? Hivi kweli munaridhia tafsiri hii?" Akajibu:
"Bila shaka wako baadhi ya Masahaba walio mlalamikia Ali na walikuwepo wenye kumchukia na kumbughudhi hivyo basi Mtume (s.a.w.) alitaka aizidishe chuki yao ndipo alipowaambia kwamba Ali ni mpenzi wenu na ni mtetezi wenu ili tu wampende na wasimkere." Mimi nikasema:
"Basi kama jambo lenyewe ni hilo, halihitaji kuwasimamisha wote na kuwasalisha kishaa kuanza kuwahutubia kwa kuwaambia: "Je, mimi siye bora kwenu kuliko nafsi zenu." Ili Mtume aifafanue maana ya Maula, na kama mambo yatakuwa kama unavyosema basi ilikuwa inawezekana kwake Mtume kuwaambia wale waliomlalamikia Ali (kumshitakia kwa Mtume) kwamba: "Ali ni kipenzi chenu na ni mtetezi wenu" na mambo yakaisha bila ya yeye Mtume kulizuwia katika jua kali kundi hilo kubwa ambalo lilikuwa na watu zaidi ya laki moja wakiwemo wazee na wanawake. Mtu mwenye akili hawezi kabisa kukubaliana na hivyo (usemavyo).


Akasema: "Je, mtu mwenye akili ataamini kwamba Masahaba laki moja hawakuifahamu maana uliyoifahamu wewe na Mashia?" Nikasema: "Kwanza wengi wao walikuwa hawakai Madina, pili hakika wao moja kwa moja walifahamu kama nilivyofahamu mimi na Mashia na ndiyo maana wanachuoni wamesimulia kwamba, Abubakr na Umar walikuwa miogoni mwa waliompongeza Ali waliposema: "Hongera Ewe mwana wa Abu Talib umekuwa mtawalia mambo ya kila muumini". Akasema: "Basi ni kwa nini hawakumpa baia baada ya Mtume kufariki? Unawaona kwamba wao waliasi na kwenda kinyume cha amri ya Mtume (Astaghfirullah) Mwenyezi Mungu anisamehe kutokana na kauli hii". Mimi nikasema:"Ikiwa wanachuoni wa Kisunni wanashuhudia ndani ya vitabu vyao kwamba baadhi yao yaani Masahaba walikuwa wakienda kinyume cha maamrisho ya Mtume zama za uhai wake tena mbele yake[36] basi siyo ajabu kuyaacha maamrisho yake baada ya kufariki kwake, na ikiwa wengi wao walimtuhumu Mtume kwa kumpa uamirijeshi Usamah bin Zaid kutokana na umri wake kuwa mdogo pamoja na kuwa jeshi hilo la Usama lilikuwa ni kwa muda mfupi basi ni vipi wao watakubali Ali awe amiri juu yao tena mwenye umri mdogo kisha kwa muda wa uhai wao (au wake) na Ukhalifa wake ni kwa kila kitu, nawe umeshuhudia mwenyewe kwamba baadhi yao walikuwa wakimchukia Ali na kumkera?

Alinijibu huku akiwa amekasirika: "Lau kama Imam Ali Karrama Llahu Waj-hahu angekuwa anafahamu kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu amemtawalisha Ukhalifa, basi asingenyamazia haki yake naye alikuwa mtu shujaa isitoshe Masahaba wote walikuwa wakimuogopa" Mimi nikasema: "Bwana wangu hii ni maudhui nyingine nami sitaki kuiingia kwani wewe hukutosheka na hadithi za Mtume zilizosahihi na unajaribu kuziawili na kuzibadilisha maana yake ili tu ulinde utukufu wa viongozi waliopita, basi mimi nitakukinaisha- namna gani suala la kunyamazia kwa Imam Ali au kutoa hoja kwake dhidi yao kuhusu haki yake ya Ukhalifa?


Yule bwana alitabasamu huku akisema: "Wallahi mimi ni miongoni mwa watu wanaomtukuza Bwana wetu Ali Karrama llahu Waj-hahu juu zaidi kuliko wengine, na lau ningekuwa na uwezo nisingemtanguliza juu yake Sahaba yeyote, kwani yeye (Ali) ndiye mlango wa mji wa elimu na ndiye simba wa Mwenyezi Mungu aliyemshindi, lakini matakwa ya Mwenyezi Mungu yanamtanguliza amtakaye na kumbakisha nyuma amtakaye, haulizwi (Mwenyezi Mungu) kile akifanyacho nao viumbe wataulizwa".


Nami nilitabasamu na nikasema: "Na hii pia ni maudhui nyengine inatutaka tuzungumzie Qadhaa na Qadar na hapo kabla tumetangulia kuizungumzia na kila mmoja wetu akawa amebakia kwenye mtazamo wake, kwa hakika ninashangaa ewe bwana wangu ni kwa nini kila ninapozungumza na mwanachuoni wa Kisunni na ninapomshinikiza kwa hoja haraka sana huikimbia maudhui tuliyonayo na kushika maudhui nyingine ambayo haina uhusiano na utafiti tunao ulenga".

Akasema: "Nami nabakia kwenye mtazamo wangu siwezi kuubadilisha." Basi nilimuaga nikaondoka, na nikabaki ninafikiri saa zote, ni kwa nini simpati mwanachuoni miongoni mwa wanachuoni wetu atakayekamilisha pamoja nami mazungumzo haya na ausimamishe mlango mguuni kwake kama isemavyo methali mashuhuri huku kwetu. Baadhi yao huanza mazungumzo na pale anapojikuta hawezi kusimamisha hoja juu ya maneno yake huepa kwa kusema, "Hao ni umati uliokwisha pita, wanayo yao waliyoyachuma nanyi munayo yenu mliyoyachuma", na baadhi yao husema: "Tunahaja gani ya kuzusha fitna na chuki, la muhimu ni kuwa Masunni na Mashia wanaamini Mungu mmoja na Mtume mmoja basi hii inatosha" Na wengine husema kwa kifupi tu, "Ewe ndugu yangu muogope Mwenyezi Mungu juu ya Masahaba". Basi je, kuna nafasi yoyote inayobakia kwa watu hawa kutafiti, kuchunguza kielimu, kuing'arisha njia na kurejea kwenye haki ambayo hapana baada yake isipokuwa upotofu? vipi) mbinu za Qur'an ambazo zinawataka watu kusimamisha dalili "Waambie leteni hoja zenu ikiwa ninyi mnasema kweli." Pamoja na kufahamu kwamba lau wao wataacha kuwashutumu na kuwahujumu Mashia basi tusingelazimika kujadiliana nao hata kwa yale yaliyo mema.


AYA YA KUKAMILISHA DINI
AYA YA KUKAMILISHA DINI PIA INAHUSIANA NA SUALA LA UKHALIFA Kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni Neema yangu na nimeuridhia kwenu Uislamu kuwa ndiyo dini" (Qur'an, 5:3) Mashia wanakubaliana kuwa ilishuka hapo Ghadir Khum baada ya Mtume (s.a.w.) kumsimika Imam Ali kuwa ni Khalifa wa Waislamu, na hiyo ni riwaya iliyopokelewa toka kwa Maimamu wa kizazi kitakatifu, na ndiyo maana utawaona (Mashia) wanauhesabu Uimamu kuwa ni miongoni mwa "Misingi ya Dini" (Usulud-Din). Pamoja na kwamba wengi wa wanachuoni wetu wa Kisunni wanaisimulia aya hii kuwa ilishuka hapo Ghadir Khum baada ya kusimikwa Imam Ali nami ninataja miongoni mwao kama mfano:

1). Tarikh Dimishq ya ibn Asakir Juz. 2 uk. 75.
2). Manaqib Ali bin Abi Talib cha Ibn Maghazili As-Shafiiuk.19.
3). Tarikh Baghaad cha Al-Khatib Al-Baghdadi Juz.8 uk. 290.
4). Al-It-Qan cha SuyutiJuz. 1 uk. 31.
5). Tadhikiratul-Khawas cha ibn Al-Jauzi uk. 30.
6). Al-Manaqib cha Al-Khawar-Zami Al-Hanafi uk. 80.
7). Tafsir ibn KathirJuz. 2 uk. 14.
8). Ruhul-Maani ya Al-Alusi Juz. 6uk. 55.
9). Al-Bidayatu Wan-Nihayah ya Ibn Kathir Juz.5 uk. 213.
10). Ad-Durrul-Manthur ya Suyuti Juz. 3 uk. 213.
11). Yanabiul-Mawaddah cha Al-Qanduzi Al-Hanafi uk. 115.
12). Shawahidut-Tanzil cha Al-Haskani Juz. 1 uk. 157.


Mimi nasema, pamoja na yote hayo wanachuoni wa Kisunni wamelazimika kuibadilisha aya hii na kuiweka kwenye munasaba mwingine, na kufanya hivyo ni kwa ajili ya kulinda heshima ya viongozi waliopita miongoni mwa Masahaba, vinginevyo kama wangekubali kwamba aya hiyo imeshuka hapo Ghadir Khum na wangekiri kwamba kutawazwa kwa Imam Ali ndiyo jambo ambalo kwalo Mwenyezi Mungu aliikamilisha dini na akawatimizia Waislamu kwa jambo hilo neema yake, na pia ungelitoweka Ukhalifa wa Makhalifa watatu ambao walimtangulia Imam Ali na ungeporomoka uadilifu wa Masahaba na hadithi nyingi zingeyeyuka kama chumvi inavyoyeyuka ndani ya maji. Lakini jambo hili haliwezekani na ni jambo zito kwani lahusika na itikadi ya umma mkubwa wenye historia yake na wanachuoni wake na watukufu wake, hivyo basi imeshindikana kwetu sisi kumpinga Bukhari na Muslim ambao wanasimulia ya kwamba aya hiyo ilishuka Ijumaa jioni ya siku ya Arafa.


Na kwa riwaya hizo za kina Bukhari zile riwaya za mwanzo zinaonekana kuwa ni uzushi wa Kishia na hazina msingi wowote wa usahihi, na kuwashutumu Mashia inakuwa ni bora mno kuliko kuwashutumu Masahaba, kwani Masahaba hawa wamehifadhika kutokana na makosa[37] na wala hapana uwezekano wa mtu yeyote kuyakosoa matendo yao na maneno yao. Amma hao Mashia wao ni majusi, makafiri, wazandiki, na ni walahidi na muasisi wa madhehebu yao ni Abdallah bin Saba[38] ambaye ni Myahudi aliyesilimu zama za Uthmani bin Affan ili kuwavuruga Waislamu na Uislamu. Kufanya hivyo ni jambo jepesi mno ili kuupotosha umma ambao umeleleka juu ya msingi wa kuwatukuza na kuwaheshimu Masahaba (yaani Sahaba yeyote yule japokuwa alimuona Mtume mara moja) basi itawezekana vipi kwetu sisi kuwakinaisha watu kwamba riwaya hizo siyo uzushi wa Kishia bali ni hadithi za Maimamu kumi na wawili ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu alitamka kuhusu Uimamu wao, Maimamu ambao serikali za Kiislamu katika karne ya kwanza zilifanikiwa kupandikiza mapenzi na kuwaheshimu Masahaba dhidi ya Ali na wanawe juu ya Mimbar na kuwafuatilia Mashia wao kwa kuwauwa na kuwafukuza, na hapo ndipo ilipoanzia chuki na karaha dhidi ya kila Shia kutokana na mambo yaliyosambazwa na vyombo vya habari katika zama za Muawiyah ikiwa ni pamoja na itikadi mbaya dhidi ya Shia, na leo hii Mashia wanaitwa kuwa ni kundi la upinzani ili tu kuwatenga na kuwamaliza.


Na kwa ajili hiyo tunawakuta hata waandishi na wanahistoria katika zama hizo wakiwaita Mashia kuwa ni Ar-Rawafidhi" (yaani wapinzani) na huwakufurisha na kuwauwa ili tu kujipendekeza kwa watawala. Ulipoanguka utawala wa Banu Umayyah na ukafuatiwa na dola ya Banu Abbas baadhi ya wanahistoria walibadili muelekeo wao, baadhi yao wakaitambua haki ya watu wa nyumba ya Mtume hiyo ni kwa sababu ya Maimamu wa nyumba ya Mtume nafsi zao zilishikamana na Akhlaq yao njema na elimu zao ambazo zilijaa ulimwenguni, na uchamungu wao na utukufu aliowapa Mwenyezi Mungu.

Kutokana na mazingira haya wanahistoria hao wakajaribu kufanya uadilifu na ndipo walipomuunganisha Ali kwenye Makhalifa waliomtangulia, lakini pamoja na hayo hawakuthubutu kuiweka wazi haki yake, na ndiyo maana utawaona hawakuandika ndani ya vitabu vyao isipokuwa sehemu ndogo tu ya ubora wa Ali na tena wanatoa zile sifa ambazo hazipingani na Ukhalifa wa waliomtangulia. Baadhi yao wameweka hadithi nyingi zinazohusu ubora wa Abubakar, Umar na Uthman kwa kupitia ulimi wa Ali mwenyewe ili wapate kukata njia ya Mashia wanaosema kuwa Ali ni bora zaidi.


Kwa kupitia uchunguzi wangu nimegundua kwamba umashuhuri wa watu na utukufu wao ulikuwa ukipimwa kwa kiwango cha kumchukia Ali bin Abi Talib, kwani Banu Umayya na Banu Abbas walikuwa wakimkurubisha na kumtukuza kila yule ambaye alikuwa akimpiga vita Imam Ali au akisimama dhidi yake kwa upanga au ulimi, ndiyo maana utawaona wanawatukuza baadhi ya Masahaba na kuwatweza wengine. Si hivyo tu bali (Banu Umayya na Banu Abbas) wakiwasheheneza kwa mali nyingi baadhi ya washairi na kuwauwa wengine, na huenda mama Aisha Ummul-Muuminina asingekuwa na hadhi kwa kiwango hicho kwa Masunni lau siyo kumchukia[39] kwake Ali na kumpiga vita.


wanaonekana wamefikia kiwango cha upuuzi na ujinga wa akili na maoni potofu kwa vile wanaitakidi juu ya Uimamu wa Mahdi anayengojewa ambaye ataujaza ulimwengu uadilifu na usawa kama ambavyo umejazwa dhulma na ujeuri. Na sasa tunarudi kuzijadili kauli za pande mbili kwa Sasa hebu turudi na tuzijadili kauli za pande mbili kwa utulivu bila ya chuki ili tufahamu ni munasaba upi na ni sababu ipi ya kushuka kwa aya ya kukamilisha dini ili itupambanukie haki na tuifuate. Hapo sasa hatuwajibiki kukubaliana na ridhaa ya hawa au chuki ya wale maadam kabla ya chochote tunaikusudia radhi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujiokoa kutokana na adhabu yake siku ambayo haitamfaa mtu mali yake wala watoto ila yule atakayemjia Mwenyezi Mungu na moyo uliosalimika. Siku ambayo nyuso zitang'ara na nyuso zingine zitakuwa nyeusi, ama wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeusi, je, mlikufuru baada ya kuamini? Basi ionjeni adhabu kwa yale muliyokuwa mukikufuru. Na ama wale ambao nyuso zao zitang'ara basi hao watakuwa katika Rehma za Mwenyezi Mungu wao wataingia humo. (Qur'an, 3:106)