ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

 

AQIDA ZA KISHIA NA KISUNNI
Miongoni mwa mambo yaliyonizidishia yakini kwamba Mashia Imamiyyah ndiyo lile kundi lenye kuokoka, ni itikadi zao bora ambazo ni nyepesi kukubalika kwa kila mwenye akili yenye hekima na hisia iliyo salama. Kwa Mashia tunakuta kila mas-ala miongoni mwa mas-ala na kila itikadi miongoni mwa itikadi inayo tafsiri inayotosheleza toka kwa mmoja wa Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.), kitu ambacho huenda tusikipatie ufumbuzi kwa Masunni na kwa vikundi vingine (vya Kiislamu). Nitazifuatilia katika mlango huu baadhi ya itikadi zilizo muhimu kwa pande zote mbili (Shia na Sunni), na nitajaribu kuonesha yale ambayo mimi nimeyakinai, na nitamuachia msomaji uhuru wa kufikiri na kuchagua na kukosoa.

Ninakumbusha tu kwamba, itikadi ya msingi kwa Waislamu wote ni itikadi moja ambayo ni kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, Malaika wake, vitabu vyake na Mitume wake. Waislamu hawamtengi yeyote miongoni mwa Mitume wa Mwenyezi Mungu kama ambavyo wanaafikiana kwamba moto ni kweli (kuwa upo) na pepo ni kweli (ipo) na kwamba Mwenyezi Mungu atawafufua waliomo makaburini na kuwakusanya siku ya hesabu.

Kama ambavyo wanaafikiana juu ya Qur'an na wanaamini kwamba Mtume wao Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kibla chao ni kimoja, lakini hitilafu ilitokea katika maf-humu ya itikadi hizi na hapo ndipo pakawa mahala pa malumbano na wakawa wana maoni mbali mbali na madhehebu mengi.


ITIKADI YA MUNGU KISHIA NA KISUNNI
ITIKADI KUMUHUSU MWENYEZI MUNGU MTUKUFU KWA PANDE MBILI (SHIA-SUNNI)
Cha muhimu kitakachoelezwa katika maudhui hii ni suala la kumuona Mwenyezi Mungu Mtukufu. Masunni wamethibitisha jambo hilo la kumuona Mwenyezi Mungu huko akhera ya kuwa waumini wote watamuona Mwenyezi Mungu.

Na tunapozisoma sihahi za kisunni kama vile Bukhari na Muslim, tunakuta zimo riwaya nyingi zinazosisitiza kumuona Mwenyezi Mungu hasa na siyo kwa majazi,[2] bali tunakuta ndani yake kuna kumfananisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na eti kwamba anacheka[3] na anakuja na kutembea, anashuka kwenye mbingu ya dunia[4] bali atafunua muundi wake ambao unayo alama atakayotambulikana kwayo[5] na ataweka unyayo wake ndani ya Jahannam nayo itajaa iseme basi basi (inatosha) na mengineyo miongoni mwa mambo na sifa ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu ametakasika nazo na mfano wa hayo.[6] Katika ukurasa wa 202 anathibitisha kwamba Mwenyezi Mungu ana mkono na vidole.


Nakumbuka kwamba wakati fulani nilipata kupita katika mji wa Lamu huko Kenya Afrika ya Mashariki, nilimkuta Imam wa Kiwahabi akiwahutubia watu msikitini anawaambia kwamba: "Mwenyezi Mungu ana mikono miwili na miguu miwili na uso". Nilipompinga juu ya hilo alisimama na kutoa ushahidi kutoka katika Qur'an akasema: "Na Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba, (sivyo bali) mikono yao ndiyo iliyofumba na wamelaaniwa kwa sababu ya yale waliyoyasema, lakini mikono ya Mwenyezi Mungu i wazi". (Qur'an, 5:64)

Na akasema tena:
"Na tengeneza Jahazi mbele ya macho yetu". (Qur'an, 11:37) Na alisema tena:
"Kila kilicho juu yake kitaondoka na utabaki uso wake (dhati yake)". (Qur'an, 55:26-27) Mimi nilisema: Ewe ndugu yangu aya zote hizi ulizozileta na nyinginezo zote ni majazi siyo hakika (kama zinavyoonesha)!! Alijibu akasema:
"Qur'an yote ni hakika wala hapana ndani yake majazi". Mimi nikasema: Kama ni hivyo basi ipo tafsiri ya aya isemayo kuwa, "Na aliyekipofu katika hii (dunia) basi atakuwa kipofu katika akhera". (Qur'an, 17:72)
Basi Je, ninyi mnaichukulia aya hii kwa maana ya hakika (kama inavyoonekana)? Kwani (inajulisha kuwa) kila aliye kipofu duniani atakuwa kipofu huko akhera"? Sheikh huyo alijibu: "Sisi tunazungumzia juu ya mkono wa Mwenyezi Mungu na jicho la Mwenyezi Mungu na uso na Mwenyezi Mungu wala kabisa hatuna habari na vipofu!!" Nikasema: Hebu na tuachane na habari ya vipofu, basi je, ni ipi tafsiri yenu kuhusu aya uliyoitaja isemayo, "Kila kitu kitaangamia isipokuwa uso wake". (Qur'an, 28:88)

Aliwageukia waliohudhuria mskitini akawaambia," hivi yuko miongoni mwenu ambaye hakuifahamu aya hii? hapana shaka kwamba ikowazi mno mfano wa ile kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo: "Kila kitu kitaangamia isipokuwa uso wake". Mimi nikasema kumwambia: "Hakika wewe umezidisha maji ndani ya unga (umezidi kuharibu), Ewe ndugu yangu, bila shaka tumehitilafiana kuhusu Qur'an, wewe umedai kwamba ndani ya Qur'an hakuna majazi bali Qur'an yote ni hakika (yaani isomekavyo ndivyo itakavyotafsiriwa) nami nimedai kwamba ndani ya Qur'an mna majazi na hasa kuhusu aya ambazo ndani yake kunaonesha kumfanyia kiwiliwili Mwenyezi Mungu au kumfananisha. Iwapo utaing'ang'ania rai yako hiyo basi itakulazimu useme kwamba kila kitu kitaangamia isipokuwa uso wake, hii ikiwa na maana kwamba mikono yake na miguu yake na mwili wake wote utatoweka na kuangamia na hakitabakia ila uso wake, na Mwenyezi Mungu ni mtakatifu mno hana sifa kama hiyo. Kisha niliwageukia waliohudhuria hapo nikawaambia, "Hivi kweli mnakubaliana na tafsiri hii (ya Sheikh huyu?)" Wote walinyamaza na Sheikh wao aliyekuwa akihadhiri naye hakusema kitu, basi nikawaaga nikatoka hali ya kuwa nawaombea uongofu na mafanikio.


yao kuhusu Mwenyezi Mungu kama ilivyo ndani ya vitabu vyao na katika mihadhara yao.Naweza tu kusema kwamba, wako baadhi ya wanachuoni wetu wa Kisunni wanaipinga itikadi hiyo lakini wengi wao wanaamini kuwa watamuona Mwenyezi Mungu huko akhera na watamuona kama wanavyouona mwezi mpevu ambao haukufunikwa na mawingu. Na kuhusu jambo hili wao hutolea ushahidi wa aya isemayo kuwa: "Siku hiyo nyuso zitang'ara zikingoja rehma ya Mola wao" (Wujuhun Yaumaidhin Nadhirah Ila Rabbiha Nadhirah)[7]. (Qur'an, 75:22)

Na kwa hakika ni kiasi tu cha wewe kuifahamu itikadi ya Mashia Imamiyyah kuhusu jambo hili, nafsi yako italiwazika na akili yako itakubaliana na taawili za aya za Qur'an zinazoonesha kuwa kuna namna fulani ya kumfanya Mwenyezi Mungu kuwa ana mwili, au kumfananisha Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kitu fulani, bali kuzichukulia aya hizo kuwa ni majazi na istiarah na siyo kama zinavyoonekana, wala dhahiri ya matamko yake kama wanavyodhani baadhi ya watu. Imam Ali (a.s.) anasema kuhusu jambo hili: "Azma ya hali ya juu haifikii kumtambua Mwenyezi Mungu, wala fahamu yenye uerevu wa hali ya juu kabisa haitomuelewa Mwenyezi Mungu jinsi alivyo. Mwenyezi Mungu ambaye sifa zake hazina mipaka ijulikanayo, hapana jinsi ya kumsifu, wala hana wakati ulio na upeo wala muda."[8]

Naye Imam Muhammad Al-Baqir katika kuwapinga wanaomshabihisha Mwenyezi Mungu anasema, "Bali kila katika undani wa maana zake, basi hicho ni kiumbe kilichotengenezwa kama sisi na kitarudishwa kwetu". Taz: Aqaidul-Imamiyyah. Na kuhusu jambo hili linatutosha jawabu la Mwenyezi Mungu ndani ya Qur'an aliposema: "Hakuna chochote chenye mfano wake". Na kauli yake nyingine "Macho hayamdiriki Mwenyezi Mungu". Pia kauli ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake Musa (a.s.) pale alipotaka amuone Mwenyezi Mungu akasema, "Ewe Mola wangu nioneshe nikuone akasema kamwe huwezi kuniona." Herufi hii ya "Lan" iliyoko kwenye aya hii inamaanisha "Kamwe, Abadan" kama wasemavyo wanazuoni wa fani ya nahau.

Yote hayo ni dalili pasina shaka yoyote juu ya kusihi kwa kauli za Mashia ambao wanategemea kauli za Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) kuhusu jambo hilo, Maimamu hao ambao ndiyo wenye undani wa elimu na nyumba yao ambayo ndiyo mahala pa utume na wao ndiyo wale ambao Mwenyezi Mungu amewarithisha elimu ya kitabu (Qur'an). Basi yeyote yule atakaye ziyada kuhusu uchunguzi huu, anawajibika kuvirejea vitabu vilivyofafanua maudhui hii kama vile kitabu kiitwacho "Kalimatun Haular-Ruuyah " cha Sayyid Shara'fud-Din mwandishi wa Al-Murajaat"[9]


ITIKADI YA UTUME KISHIA NA KISUNNI
Tofauti iliyopo baina ya Shia na Sunni katika mlango huu ni maudhui inayohusu "Ismah " (kuhifadhika kutokana na makosa). Mashia wanakubali Ismah kwa Manabii (a.s.) kabla ya kutumwa kwao na baada ya kutumwa. Masunni wanasema kwamba, Manabii ni Maasum (wamehifadhika) tu katika yale wanayoyafikisha miongoni mwa maneno ya Mwenyezi Mungu, ama yasiyokuwa hayo wao ni kama watu wengine wanakosea na kupatia, na wamenakili riwaya nyingi kuhusu jambo hilo ndani ya vitabu vyao zinazothibitisha kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) alikosea katika minasaba mingi. Kulikuweko baadhi ya Masahaba wakimsahihisha kama vile kwenye qadhiya ya mateka wa Badri ,qadhiya ambayo Mtume alikosea na Umar akapatia, na lau siyo yeye Umar basi Mtume wa Mwenyezi Mungu angeliangamia.


Taz: Albidayatu Wan-Nihaya cha Ibn Kathir, naye amenakili kwa Imam Ahmad na Muslim na Abu Dawud na Tirmidhi. Na miongoni mwa riwaya hizo ni ile isemayo kuwa, Mtume alipofika Madina aliwakuta watu wa hapo wakiipandisha mitende akawaambia, "Msipandishie baadaye zitakuwa tende". Yakatokea mavuno hafifu (walipokuwa wameacha kuipandishia), watu wa Madina wakaja wakamlalamikia juu ya hilo. naye Mtume akawaambia, "Ninyi ni wajuzi wa mambo ya dunia yenu kuliko mimi". Katika riwaya nyingine aliwaambia, "Bila shaka mimi ni mtu tu, basi nitapokuamuruni jambo fulani katika dini yenu ichukueni, na nitapokuamuruni jambo fulani kwa maoni yangu basi mimi ni mtu tu (chunguzeni)". Taz: Sahihi Muslim Kitabul-Fadhail Juz. 7 uk. 95, Musnad ya Imam Ahmad Juz. 1 uk. 162 na Juz. 3 uk. 152.

Na kuna wakati Masunni wanasimulia kuwa Mtume (s.a.w.) alifanyiwa uchawi na akabakia katika hali hiyo ya kufanyiwa uchawi kwa siku kadhaa akiwa hajuwi alitendalo mpaka akawa hudhania kwamba yeye huenda kwa wakeze kumbe hawaendei.[10] Au hudhani amefanya kitu fulani kumbe hakukifanya.[11] Na kuna wakati wanasimulia kuwa, alisahau ndani ya sala yake hakufahamu ni rakaa ngapi ameswali[12] na kwamba yeye Mtume alilala akapitiwa na usingizi mpaka kukasikika kukoroma kwake kisha akaamka na akasali bila ya udhu.[13] Na wanasimulia kwamba Mtume hukasirika na kumtukana na kumlaani asiyestahiki hilo kisha husema: "Ewe Mwenyezi Mungu bila shaka mimi ni mtu tu, basi Muislamu yeyote niliyemlaani au kumtukana, mfanyie hiyo kwake iwe ni zaka na rehma.[14]


Na wanasimulia kwamba Mtume alikuwa amelala nyumbani kwa bibi Aisha mapaja yakiwa wazi, Abubakr akaingia Mtume akazungumza naye akiwa katika hali ile ile, kisha aliingia Umar na akazungumza naye na Mtume akiwa katika hali ile ile, na alipobisha hodi Uthman Mtume akarekebisha nguo zake, bibi Aisha alipomuuliza Mtume juu ya kufanya kwake hivyo, Mtume akamwambia bibi Aisha:
"Basi ni kwa nini nisimstahi mtu ambaye Malaika walimstahi."[15] Pia wanasimulia kwamba, Mtume alikuwa akiamka na janaba katika mwezi wa Ramadhan[16] na sala ya asubuhi humpita.Basi na mambo mengineyo mengi miongoni mwa hadithi ambazo akili haiwezi kuzikubali wala dini na hata muruwa wa mtu hauwezi kukubaliana."[17]

Ama Mashia kwa kuwategemea Maimamu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.) wao wanawatakasa Mitume kutokana na uzushi huu na mwingine aliozushiwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) na Mashia wanasema ya kwamba, "Mtume ametakasika kutokana na makosa, madhambi na maasi madogo au makubwa, naye ni maasum (amehifadhiwa) kutokana na kukosea, kusahau na kughafilika na amehifadhiwa dhidi ya uchawi na kila kitu kinachovuruga akili, bali yeye ametakasika mno na hata yale yote yasiyokubaliana na muruwa na tabia njema kama vile kula njiani, au kucheka kwa sauti ya juu au mzaha usiyostahiki au kitendo chochote kinachochukiza kukitenda kwa mujibu wa jamii inavyofahamu, bali wachilia mbali kuweka shavu lake juu ya shavu la mkewe mbele za watu na kuangalia yeye na mkewe mchezo wa Masoudani.[18] Wakati mwingine wanasema eti Mtume humtoa nje mkewe kwa kusudi la kushindana naye, basi kuna wakati Mtume humshinda mkewe na mara nyingine mke aibuke mshindi dhidi ya Mtume, kisha Mtume amwambie mkewe: "Ushindi huu ni mahali pa ule"![19]

Mashia wanaziona riwaya kama hizi zinazopingana na Ismah ya Manabii kuwa riwaya za uzushi zilizozushwa na Banu Umayyah na wasaidizi wao. Kwanza, kwa lengo la kuiporomosha heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na pili, ili tu wapate sababu ya kuhalalisha matendo yao machafu na makosa yao ambayo historia imeyasajili, kwani ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu anakosea na anapondokea kwenye matamanio kama walivyosimulia katika kisa cha Mtume kumtamani bibi Zainab binti Jahshi pindi alipomuona akichana nywele zake hali ya kuwa ni mke wa Zaidi bin Harithi eti Mtume alisema: "Umetukuka ewe Mwenyezi Mungu mwenye kugeuza nyoyo."[20] Au kile kisa cha Mtume kumpenda mno bibi Aisha na kukosa uadilifu kwa wakeze wengine mpaka kuna wakati fulani wakamtuma bibi Fatmah (a.s) na wakati mwingine bibi Zainab binti Jahshi ili kumtaka afanye uadilifu.[21] Basi ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ndiyo yuko katika hali kama hii, Muawiyah bin Abi Sufiyan, Mar-wan bin Al-Hakam na Amr bin Al-A's na Yazid bin Muawiyah na Makhalifa wote ambao walitenda maovu na kuvunja heshima za vitu vitakatifu na wakawauwa watu bila makosa watakuwa hawana lawama (kutokana na movu hayo waliyoyafanya).


Maimamu watokanao katika nyumba ya Mtume (s.a.w.) ambao ndiyo Maimamu wa Mashia wao wanasema kuwa, Mtume (s.a.w.) ni Maasum na huzipa tafsiri aya za Qur'an ambazo dhahiri yake hufahamisha kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu alimkemea Mtume wake kama vile aya ya "Abasa Watawalla" au zile ambazo baadhi yake huonesha kuthibitisha kuwa Mtume anayo madhambi kama asemavyo Mwenyezi Mungu "Ili Mwenyezi Mungu akusamehe madhambi yako yaliyotangulia (hapo kabla) na yale yajayo" Au kama vile kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
"Bila shaka Mwenyezi Mungu amemsamehe Mtume" (Laqad Taaba LLahu Ala Nnabi) na ile isemayo, "Mwenyezi Mungu amekusamehe kwa wewe kuwaruhusu.


Na aya zote hizi haziangushi "Ismah" ya Mtume (s.a.w.), kwani baadhi ya aya hizo Mtume siye aliyekusudiwa kwenye aya hizo na nyingine huchukuliwa kuwa ni majazi na siyo kama dhahiri ya matamko ilivyo, na jambo hilo (la kuweko majazi) latumika mno katika lugha ya Kiarabu na Mwenyezi Mungu amelitumia katika Qur'an Tukufu. Na yeyote atakaye ufafanuzi na kupata uhakika wa mambo hayo, basi anawajibika kuvirejea vitabu vya Tafsiri vya Mashia kama vile "Almizan Fi Tafsiril-Qur'an ya Allamah Attabatabai na Tafsirul-Kashif ya Muhammad Jawad Mughniya, na Al-Ihtijaj ya Tabrasi na wengineo, 136 Babu Fadhail Aisha.

kwani mimi nimeleta kwa ufupi na kuonesha itikadi za pande hizi mbili kwa ujumla, na lengo la kitabu hiki siyo jingine isipokuwa ni kubainisha kukinaika kwangu binafsi ambako nimekinaika, na ni uchaguzi wangu binafsi wa Madhehebu yale yasemayo kuwa Mitume ni "Maasum" na Mawasii wao baada ya Mitume ni "Maasum ". Na itikadi hii inaifanya akili yangu iwe na raha na kuniondoshea mashaka na utatanishi. Na kusema eti Mtume anakuwa Maasum tu katika kufikisha maneno ya Mwenyezi Mungu hii ni kauli mbaya isiyokuwa na hoja ndani yake, kwani hakuna dalili inayoonesha kwamba sehemu hii katika maneno ya Mtume ndiyo iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu na sehemu ile ni maneno yatokayo kwake mwenyewe. Basi vipi iwe katika yale ya mwanzo ni Maasum na katika yale ya pili asiwe Maasum hivyo uwepo uwezekano wa kuwa na makosa ndani yake.


Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kauli hii inayojichanganya, kauli ambayo inasababisha kuleta shaka na tuhuma kuhusu utakatifu wa dini. Na jambo hili linanikumbusha majadiliano yaliyopita kati yangu na jamaa fulani miongoni mwa marafiki zangu baada ya mimi kuuona ukweli, na nilikuwa nikijaribu kuwakinaisha kwamba Mtume (s.a.w.) ni Maasum, nao walikuwa wakijaribu kunikinaisha kwamba Mtume ni Maasum tu katika kufikisha Qur'an, na miongoni mwao alikuwemo mtaalam kutoka "Tuzad" "Sehemu ya Al-Jarid" nao jamaa wa kutoka sehemu hiyo wanafahamika sana kwa akili pevu na elimu na utambuzi wa ajabu. mtaalam huyo alifikiri kidogo kisha akasema: "Enyi jamaa, mimi ninayo maoni fulani kuhusu mas-ala haya".

Basi sote tukasema: "Tafadhali leta maoni uliyonayo". Akasema: "Hakika haya ayasemayo ndugu yetu Tijani kwa niaba ya Mashia ni kweli na ndiyo sahihi, na sisi tunawajibika kuitakidi kuwa Mtume ni maasum moja kwa moja vinginevyo tutaingiza mashaka ndani ya Qur'an yenyewe!! Wale jamaa wengine wakasema: "Kwa vipi itakuwa hivyo"?
Yeye alijibu kwa haraka aksema: "Hivi mmepata kuikuta sura yeyote miongoni mwa sura za Qur'an kwamba mwishoni mwake kuna uthibitisho wa Mwenyezi Mungu Mtukufu"?
Na anakusudia uthibitisho kuwa ni:"Muhuri ambao huhitimishiwa mapatano na barua Hi kuonesha uhakika wa muhusika na kwamba barua hiyo inatoka kwake". Basi jamaa hao wote walicheka tu kutokana na utambuzi huu wa ajabu lakini wenye maana kubwa sana. Lakini mtu yeyote asiyekuwa na chuki atazingatia kwa akili yake na ukweli utamgonga tu, na ukweli huo ni kuwa: "Kuitakidi kwamba Qur'an ni maneno ya Mwenyezi Mungu ni kuitakidi Ismah ya yule anayeifikisha moja kwa moja bila ya kugawa (Ismah yake kuwa ni ya nyakati fulani tu na nyakati zingine inatoweka) kwani haiwezekani kwa yeyote kudai kwamba alimsikia Mwenyezi Mungu akizungumza, na wala hawezi yeyote akadai kuwa alimuona Jibril wakati akiteremka na wahyi.


Kwa kifupi kauli ya Mashia kuhusu Ismah ni kauli ya sawa na kwayo hiyo hutuliza na kuondosha wasi wasi wa nafsi na ushawishi wa shetani na inakata kabisa njia ya wachochezi wenye fitna hasa maadui wa dini miongoni mwa Wayahudi na Wakristo na Walahidi ambao hutafuta vipenyo vya kupitia ili kuvuruga itikadi zetu na dini yetu na kumshambulia Mtume wetu. Basi mara nyingi utawaona wanatoa hoja dhidi yetu kwa kutumia yale yaliyomo ndani ya Sahih Bukhari na Muslim miongoni mwa matendo na maneno ambayo hunasibishwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu hali ya kuwa Mtume yu mbali mno nayo (hakusema hayo wala hakutenda).[22]

Basi tutafanyaje ili tuwakinaishe kwamba kitabu cha Bukhari na Muslim ndani yake kuna mambo ya uzushi, na jambo hili bila shaka ni gumu kwani Masunni hawalikubali kwa kuwa Bukhari kwao wao ni kitabu sahihi mno baada ya kitabu cha Mwenyezi Mungu!22