HADITHI ZA MTUME (S.A.W.W)PAMOJA NA MAIMAMU (A.S)

 
RIBA
. Dhambi la riba ni miongoni mwa Madhambi Makuu. . Kwa mujibu wa Qur'an tukufu, kuchukua riba ni dhambi ambalo linasababisha adhabu kali kabisa kutoka kwa Allah swt. Adhabu za kuchukua na kutoza riba ni kali kabisa kuliko madhambi mengine. Kama ilivyoelezwa katika Surah Aali Imran, 3, : 130 - 131: 'Enyi Mlioamini! Msile riba, mkizidisha mara dufu kwa mara dufu; na mcheni Allah ili muweze kuwa na ufanisi' 'Na ogopeni moto wa Jahannam ambao umetayarishiwa makafiri.' . Allah swt anatuambia katika Qur'an Tukufu, Surah al Baqarah, 2, Ayah 275 : 'Wale wanaokula riba, hawasimami ila kama anavyosimama yule ambaye Shaitani kamzuga kwa kumsawaa; na haya ni kwa sababu wamesema, 'biashara ni kama riba', Allah ameihalalisha biashara na kaiharamisha riba. N a aliyefikiwa na mauidha kutoka kwa Mola wake, kishaakajizuia, basi yamekwisha mthibitikia yale (mali) aliyoipata; na hukumu yake iko kwa Allah. Lakini wanaorejea (kula riba) basi hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele.'


. Ayah hiyo inatuthibitishia kuwa wale wanaochukua riba watabakia kwa milele katika Jahannam (Motoni) na kamwe hakutakuwa na uwokovu kwa ajili yao. Allamah Muhammad Husain Tabatabai (a.r.) katika Tafsiri ya Al-Mizan , anasema: "Adhabu aliyoiweka Allah swt kwa ajili ya mla riba ni kali kabisa kwani hakuna mahala pengine palipozungumzwa kwa ajili ya wale wavunjao kutoka Furu-i-Diin. Kosa lingine ni lile la kulea urafiki pamoja na maadui wa Islam. Athari za riba zipodhahiri na bayana kwetu sote. Kukusanya na kuficha mali ndiko kunako ongezea tofauti kati ya tabaka la masikini na tajiri.Umasikini ni ugonjwa ambao unamdhalilisha na kumshusha hadhi mgonjwa wake, unateketeza uthamini wake na kuharibu maadili yake. Na haya yanaelekeza katika mutenda maovu, uizi, ubakaji na mauaji. Walanguzi ndio watu wanaowajibika kwa kuteketea kwa usawa wa kijamii, ambao wamejilimbikizia mali kupita kiasi kwamba haiwafikii wanao hitaji na wenye dharura. Kwa kuvunjika kikamilifu kwa mshikamano wa kijamii unaweza kuzua na kukuza vita vya wenyewe kwa wenyewe au vita vya ndani na kuendelea hadi kuzuka kwa vita vya dunia ambavyo hatima yake itakuwa ni mauaji na maangamizo. Katika ulimwengu wa sasa ikiwa na silaha za kisasa za teknolojia ya hali ya juu na ya maafa makubwa katika nuklia na kemikali, vita vinapozuka si kwamba vinaleta mauaji ya wanaadamu tu bali humgeuza yeye kuwa ni picha tu, mgonjwa na asiye na uwezo wowote na ameharibika kimwili kwa vizazi na vizazi vijavyo.


. Katika kitabu 'Islam and World Peace' imeandikwa: "Islam inasema kuwa mapato ya mtu yatokane na kiwango cha juhudi na kazi iliyofanyika." Kwa sababu uwekezaji wenyewe haufanyi kazi wala jitihada ya aina yoyote ile. Hivyo, mali ya matajiri haitakiwi kamwe kuongezeka kwa kutokana na riba."


. Mtume Muhammad s.a.w.w. anasema katika Hadith moja, katika Wasa'il al-Shiah : "Ibada inayo sehemu sabini. Na muhimu kabisa ni mtu kujipatia kipato chake kilicho halali." . Vile vile Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, katika Muhajjatul Baidha : "Mfanyabiashara mwaminifu atahesabiwa pamoja na Mitume a.s. Siku ya Qiyama. Uso wake utakuwa uking'ara kama mbalamwezi."


. Qur'an Tukufu inarejea kutuambia katika Qur'an Tukufu, Surah al-Baqarah, 2 Ayah 275 : ''Na aliyefikiwa na mauidha kutoka kwa Mola wake, kishaakajizuia, basi yamekwisha mthibitikia yale (mali) aliyoipata; na hukumu yake iko kwa Allah. Lakini wanaorejea (kula riba) basi hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele.' . Ayah ya hapo juu ya Qur'an inaendelea Qur'an Tukufu, Surah al-Baqarah, 2 Ayah 276 : 'Allah huyafutia (baraka mali ya ) riba: na huyatia baraka (mali yanayotolewa) sadaqa . Na Allah hampendi kila kafiri (na) afanyaye dhambi.' . Qur'an Takatifu inatuambia Surah al-Baqarah, 2, Ayah 278 : 'Enyi Mlioamini ! Mcheni Allah, na acheni yaliyobakia katika riba, ikiwa mmeamini.'


. Ushahidi wa imani ya mtu katika utiifu wa Hukumu za Allah swt, ayah hiyo hiyo inaendelea : Qur'an Tukufu, Al-Baqarah, 2, Ayah 279 'Na kama hamtafanya hivyo, basi fahamuni mtakuwa na vita na Allah na Mtume Wake….' . 'Na mkiwa mmetubu, basi matapata rasilimali zenu; msidhulumu wala msidhulumiane.' . Vile vile Mtume Muhammad s.a.w.w. amezungumzi katika hotuba yake huko Makkah : "Muelewe kuwa riba iliyokuwa imekusanywa katika zama za ujahiliyya sasa imesamehewa kabisa. Kwanza kabisa mimi binafsi nina wasameheni ile riba ( iliyopo shingoni mwenu) ya (mjombangu) ''Abbas ibn Abdul Muttalib."


. Imeripotiwa kutoka Al-Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa, katika Al-Kafi : "Kuchukua Dirham (au pesa moja) kama riba ni vibaya sana machoni mwa Allah swt kuliko kuingiliana na mwanamke aliyeharamishwa kwako." . Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Wasa'il al-Shiah : "Mtume Muhammad s.a.w.w. amemlaani vikali yule ambaye anayekubali riba, anayelipa riba, aneyeinunua riba, anayeiuza riba, yule anayeandika mikataba ya riba na yule anayekuwa shahidi wa mikataba hiyo."

. Ibn Baqir anaripoti kuwa Al-Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. alijulishwa kuhusu mtu mmoja aliyekuwa akitoza na kupokea riba kama ndiyo halali kama vile ilivyo halali maziwa ya mama. Kwa hayo, alisema Al-Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. katika Al-Kafi : "Iwapo Allah swt atanipa uwezo mimi juu ya mtu huyu, basi nitamkata kichwa." . Sama'a anasema kuwa yeye alimwuliza Al-Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. je ni kwa nini Allah swt ametaja kuharamishwa kwa riba mahala pengi katika Qur'an. Al-Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. alimjibu, Wasa'il al-Shiah : 'Ili kwamba watu wasiache tendo la kutoa misaada (kama vile kutoa mikopo bila ya riba)."

. Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. katika Wasa'il al-Shiah : "Shughuli mbaya kabisa ni ile ambayo inahusisha riba." . Zurarah anasema kuwa yeye alimwuliza Al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. kuhusu Ayah ya Qur'an isemayo katika Qur'an Tukufu, Surah Al-Baqarah,2, Ayah 276: ''Allah huyafutia (baraka mali ya ) riba: na huyatia baraka (mali yanayotolewa) sadaqa .'


. Na akaongezea kusema : "Lakini mimi ninaona kuwa mali na utajiri wa watoza riba inaendelea kuongezeka tu kila siku." . Amesema Al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. katika Wasa'il al-Shiah : "Loh ! hasara inawezekana kuwa kubwa sana ? Kwa merejeo ya Dirham moja yeye anaipoteza Dini yake. Na iwapo yeye atafanya Tawba humu duniani basi kutafikia mwisho kwa mali aliyoichuma humu duniani kwa njia iliyo haramu na hivyo kuwa fukara." . Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, katika Mustadrakul Wasa'il : "Yule anayechukua riba basi Allah swt atalijazatumbo tumbo lake kwa moto kiasi hicho hicho. Iwapo yeye amechuma zaidi kwa kutokana na mapato ya riba, basi Allah swt hatakubalia matendo yake mema. Hadi kwamba kiasi cha punje moja kama kitabakia ambacho kimepatikana kwa njia ya riba. Allah swt pamoja na Malaika Wake wataendelea kumlaani huyu mtu."


. Vile vile Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema : "Usiku wa Mi'raj Mimi niliwaona baadhi ya watu waliokuwa wakijaribu kusimama lakini hawakuweza kufanikiwa kwa sababu ya matumbo yao makubwa, niliuliza, 'Ewe Jibraili ! Je ni watu gani hawa ?' . Jibraili alijibu : "Hawa ndio wale waliokuwa wakichukua riba. Sasa wao wanaweza kusimama tu kama wale waliokamatwa na Mashetani." . Mtume Muhammad s.a.w.w. aliendelea, "Na hapo nikawaona wao wakikusanywa katika njia za wafuasi wa Firauni. Kwa kuona uchungu wa joto la Moto mkali, wao walipiga kelele : 'Ewe Allah swt ! Je Qiyama itakuwa lini ?' (Hivyo imekuwa dhahiri kuwa Moto unaozungumziwa katika riwaya hii ni adhabu katika Barzakh ).


. Imepokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad s.a.w.w. akisema, katika Mustadrakul Wasa'il : "Wakati zinaa na riba vitakapokuwa ni vitu vya kawaida katika mji wowote basi Allah swt huwapa ruhusa Malaika kuwaangamiza wakazi wake." . Ipo riwaya nyingine isemayo kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, katika Mustadrakul Wasa'il kuwa : "Utakapofika wakati Ummah wangu utaanza kutoza na kupokea riba, basi mitikisiko na mitetemeko ya ardhi yatakuwa yakitokea mara kwa mara." . Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, Wasa'il al-Shiah : "Iwapo mtu atazini pamoja na mama yake katika Al-Ka'aba tukufu, basi dhambi hili litakuwa hafifu mara sabini kuliko tendo la kutoza na kupokea riba." . Amesema al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. katika Wasa'il al-Shiah : "Katika macho ya Allah swt, kuchukua Dirham moja ya riba ni mbaya kabisa hata kuliko matendo thelathini ya kuzini pamoja na maharimu wake yaani baba kuzini pamoja na binti yake."


USAMEHEVU
. Kwa upande mmoja Uislamu unawasisitiza Waislamu kutafuta nyenzo za kujipatia mahitajio yao ya kila siku katika maisha yao kwa njia zifuatazo: . Ibada ni za aina saba, na mojawapo ni kule kujitafutia mahitaji ya kila siku kwa njia zilizo halalishwa katika Dini. . Yeyote yule aliye na maji pamoja na ardhi katika uwezo wake, na wala halimi katika ardhi hiyo, na iwapo atakumbwa na hali ya kukosa chakula cha kujilisha yeye pamoja na familia yake, basi atambue wazi kuwa huyo amekosa baraka za Allah swt. . Moja ya matendo yaliyo bora kabisa ni kilimo kwani mkulima anajishughulisha katika kilimo na upandaji wa mazao ambayo yanawafaidisha wote bila ya kuchagua iwapo huyu ni mwema au mwovu. . Yeyote yule asiyejitafutia mahitaji yake ya maisha basi kamwe hatakuwa na maisha ya mbeleni kwani atateketea. . Na yeyote yule anayejitahidi kwa bidii kubwa kwa kujipatia mahitaji kwa ajili ya familia yake basi huyo ni sawa na yule ambaye anapigana vita vya Jihad.


. Kwa upande wa pili, Islam inaamini kuwa iwapo mtu atakuwanavyo mali na milki, kilimo na viwanda, utajiri na starehe lakini bila ya Taqwa ya Allah swt kama vile imani juu ya Allah swt na Mitume a.s, Imani juu ya siku ya Qiyama, thawabu, na adhabu na bila ya kuwa na tabia njema na kuuthamini ubinadamu kama vile msamaha, ushirikiano katika mambo mema, moyo wa utoaji, kuonea huruma n.k. basi kamwe haviwezi kumpatia maendeleo. . Allah swt anatuambia katika Qur'an Tukufu Surah Al A'S'R, 103 : Ayah 1-3 " 'Naapa kwa alasiri.' " ' Hakika mwanadamu yumo hasarani !' " ' Ila wale ambao wameamini wakatenda mema na wakausiana kwa haki na subira.'


. Imam Hussein a.s. amenakiliwa akisema: "Kama kwa kweli kuna milki ya mali ya mtu humu duniani, basi hiyo ni kuwa na tabia njema. Iwapo watu wote watakufa, basi kifo jema kabisa mbele ya Allah swt ni kule kujitolea mhanga katika njia ya Allah swt." . Usamehevu upo wa aina mbili: " Sisi tunamsamehe mtu pale tunajikuta kuwa hatuna uwezo wa kulipiza kisasi. Kwa hakika aina hii ya usamehevu unatokana na subira na kuvumilia na kamwe si kusamehe. Kwa maneno mengine, ni aina mojawapo ya kutoweza kujisaidia na udhaifu. " Sisi tunamsamehe mtu ingawaje tunao uwezo wa kulipiza kisasi. Aina hii ya usamehevu ndio unaofundishwa na Islam pamoja viongozi wetu.


. Amesema Al-Imam Ali as. : "Mtu anayestahiki kusemehe wengine ni yule ambaye ni mwenye uwezo mkuu zaidi katika kuwaadhibu wengine." . Katika wusia wake wakati akiongea na Harith Hamdani, Al- Imam Ali a.s. alisema: "Tuliza ghadhabu zako na kumsamehe mtu aliyekukosea wakati wewe ukiwa na uwezo au cheo chako." "Wakati wewe utakapomzidi nguvu adui yako, basi zingatia kumsamehe ikiwa ndiyo shukurani ya kupata uwezo huo."

. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. "Kuwasamehe wengine wakati mtu yupo katika madaraka ni sambamba na tabia na desturi za Mitume a.s pamoja waja wema." . Baadhi ya Ayah za Qur'an tukufu zizungumziazo maudhui haya: Qur'an Tukufu, Sura Al- A'araf (7) Ayah ya 199, Uchukulie kusamehe na kuamrisha mema na kujiepusha na majaheli Vile vile Allah swt anatuambia katika Qur'an Tukufu, Sura A'araf ( 7 ) Ayah ya 200, 'Na iwapo wasiwasi wa Shaitani utakusumbua basi jikinge kwa Allah, Yeye ndiye Asikiaye na Ajuaye yote.'


. Qur'an Tukufu, Sura Aali 'Imran ( 3 ) Ayah 134 'Wale wanaotumia wakiwa katika hali nzuri na dhiki na ambao huzuia ghadhabu zao na kusamehe (makosa ya) watu ; kwani Allah huwapenda wafanyao mema.' . Allah swt anatuambia katika Qur'an Tukufu, Sura Aali 'Imran ( 3 ) Ayah ya 159 kuwa: Hivyo kutokana na Rehema itokayo kwa Allah kuwa wewe umekuwa mlaini kwao na kama ungalikuwa mkali na mwenye moyo mgumu bila shaka wangalikukimbia. Basi uwasamehe wewe na uwaombe msamaha na ushauriane (kwa kuwaridhisha tu ) nao katika mambo. Na unapoazimia mtegemee Allah, Hakika Allah huwapenda wamtegemeao.


Aya hii tukufu imewateremkia kuhusu wale ambao walikwenda kinyume na amri ya Mtume Muhammad sa.w.w. katika Vita vya Uhud ambapo kulisababisha Waislamu kushindwa. Watu hao walikuwa ni hamsini na wawili (52) kwa idadi ambao waliwekwa na Mtume s.a.w.w. kulinda pakuingilia huko bondeni na aliwaambia : " Iwapo sisi tutashinda au kushindwa, nyinyi kamwe musisogee wala kuondoka hata hatua moja kutoka sehemu hii iliyo nyeti." Mbinu hii ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ikiwa pamoja na baraka za Allah swt na moyo wa kujitolea mhanga wa vijana wa Kiislamu wenye imani halisi, iliwafanikisha kuwashinda maadui ambao walikimbia. Wailsamu baada ya maadui kukimbia, walianza kukusanya mali iliyopatikana vitani hapo katika uwanja wa mapigano.


Mara hawa watu hamsini na wawili walipopata habari kuwa Waislamu wameshinda na wanakusanya mali iliyopatikana vitani, wote, isipokuwa kumi na wawili tu, waliacha ngome zao wazi na kukimbilia mali huku wakiwa wamevunja amri ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. iliyokuwa imewakataza wasiondoke hapo walipo katika sura yoyote ile ama iwe ya ushindi au kushindwa. Kwa kuona haya, Khalid ibn Walid, ambaye alikuwa ni kamanda wa jeshi la makafiri, alikwenda hapo bondeni akiwa na jeshi la wapanda farasi mia mbili (200 ) wakiwa wamejiandaa kwa silaha.


Makafiri hao waliwashambulia kwa ghafla Waislamu kumi na wawili na kuwaua wote na wakatokezea kwa nyuma kushambulia jeshi la Waislamu. Katika mapigano haya, Mashujaa sabini ( 70 ) wa jeshi la Waislamu waliuawa, akiwemo Hamzah ush-Shuhadaa ( kiongozi wa mashahidi). Na Mas'ab ibn Umair vile vile wapiganaji wengi walijeruhiwa akiwemo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. pamoja na Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. Kwa hakika kuvunja amri ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. kwa hao wachache kulileta maafa makubwa kwa upande wa Waislamu. Watu walitegemea kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. atatoa amri kali kabisa dhidi ya hawa wachache; lakini sivyo na badala yake kuliteremka Ayah tukufu ikisema:


. Qur'an Tukufu, Sura Aali 'Imran ( 3 ), Ayah ya 159, kuwa: '…Basi uwasamehe wewe na uwaombe msamaha na ushauriane (kwa kuwaridhisha tu ) nao katika mambo….' . Kwa kuiteremsha Ayah hii, Allah swt alimwamuru Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. atoe msamaha kwa waliokuwa wamekosa. . Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema: "Bora ya tendo lililo mbele ya Allah swt ni kusamehe mtu ambaye amekukosea, kuwapenda ndugu na jamaa ambao wameukata uhusiano pamoja nawe, na kuwa mkarimu kwa yule ambaye aliwahi kukunyima. " Na hapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliisoma Ayah hii ya Qur'an:


. Qur'an Tukufu, Sura Al- A'araf (7) Ayah ya 199, 'Uchukulie kusamehe na kuamrisha mema na kujiepusha na majaheli' . Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. katika mkataba aliokuwa amemwandikia Malik-i-Ashtar, aliandika: "Zijazeni nyoyo zenu kwa huruma, uwema na kuwapenda waliochini yenu. Na kamwe musitendee kama wanyama walafi na waroho, kujifanya kama munawalea kwa kuwatenga, kwani wao wapo wa aina mbili: ama wao ni nduguzo katika imani au wapo sawa katika kuumbwa. Wao wanapotoka bila ya kujua na kasoro zinawaghalibu, wanakosa makosa ama kwa makusudi au bila kukusudia. Kwa hivyo nawe pia uwasamehe kwa kutegemea naye Allah swt atakusamehe, kwani wewe umekuwa na uwezo dhidi yao, na Yule aliyekuchagua wewe yu juu yako, na Allah swt yupo juu ya yule aliyekuweka katika wadhifa huu."


. Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. : "Kusikitika baada ya kutoa msamaha ni afadhali ya kufurahi baada ya kuadhibu." . Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika Hadith 'Arbain, ananakili Marehemu Deilami: "Siku ya Qiyama, mpiga mbiu atasimama na kusema: 'Yeyote aliye na malipo yake kwa Allah swt basi asimame.' Lakini hakuna watakao simama isipokuwa wale tu ambao walikuwa ni wasamehevu. Anaendelea kusema 'Je hao hawakusikiaga ahadi iliyokuwa imetolewa na Allah swt :

. Qur'an Tukufu,Surah Ash-Shuura ( 42 ), Ayah 40, 'Na malipo ya uovu mfano wa huo. Lakini anayesamehe na kusahihisha; ujira wake uko kwa Allah swt. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.' 1421. Qur'an Tukufu,Sura An-Nahl (16) Ayah 126, 'Na mkilipiza, basi lipizeni sawa na vile mlivyoonewa, na kama mkisubiri basi hiyo itakuwa bora kabisa kwa wafanyao subira'. . Baada ya ufunuo wa Ayah hiyo, Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alisema : "mimi nitakuwa mwenye subira."


. Qur'an Tukufu, Surah Fat-h (48 ) Ayah 1-2, 'Bila shaka tumekwishakupa kushinda kuliko dhahiri. Kwamba Allah alinde kwa ajili yako (dhidi) ya yale yaliyopita kabla ya (wafuasi wako) kasoro zako na yale yanayokuja …' . Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliisoma Ayah ifuatayo : Qur'an Tukufu, Surah Bani- Israil (17 ) Ayah 81, ' Na sema : 'Ukweli umefika; na uongo umetoweka; Kwa hakika uongo ndio wenye kutoweka.'


. Vile vile Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimsamehe mtumwa wa Kihabeshi, Wahshi, ambaye ndiye aliyekuwa amemwua Bwana Hamza, babake mkubwa wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. . Alimsamehe wakati ambapo alikuwa na uwezo kamili wa kumwadhibu na kulipiza kisasi. Kwa hakika hii ndiyo iliyokuwa kanuni ya mtu ambaye alikuwa akiwaambia watu wote kuwa huruma ipo imefungamana katika tabia tatu: " Kumsamehe yule aliyekutendea yasivyo sahihi. " Kudumisha mshikamano wa udugu pamoja na jamaa ambaye ameuvunja uhusiano pamoja nawe. " Kumsamehe yule ambaye amekudhulumu au kukunyima haki yako.


. Qur'an tukufu inawatakata Wailsamu waigize tabia na mwnenendo kama Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na ndiye awe kiigizo chao : . Qur'an Tukufu, Surah Ahzab (33 ) Ayah 21, Kwa hakika mnao mfano mwema kwa Mtume wa Allah, …


Kwa mujibu wa Ayah hiyo, iwapo sisi tutapenda kuwa Waislamu wema, basi itatubidi kuzifuata tabia na mienendo yote ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. . . Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. "Allah swt hakubakiza chochote kile ambacho waja Wake watakihitaji hadi Siku ya Qiyama, isipokuwa vyote vipo katika kitabu kitakatifu cha Qur'an na ambayo yote yamefikishwa kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.. Yeye amewekea mipaka kwa kila kitu, na kuweka uthibitisho kwa ajili yake. Kwa wale watakaopita mipaka yake, Allah swt ameainisha adhabu za kutubu za Kidini."


. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alisema : "Tofauti baina ya Waislamu na jamii zingine ni kwamba watu wote ni sawa mbele ya Shariah za Allah swt. Islam haitofautishi baina ya tajiri na masikini, au baina ya mwenye nguvu na mnyonge. Kwa kiapo cha Allah swt ! Lau Fatima binti ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. angalikuwa amefanya uizi, basi Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. angalimkata mkono wake pia."


AHADITH MCHANGANYIKO
. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. katika Yanabiul Mawaddah, uk. 584 na 485 : "Mimi ni mbora wa Manabii na Ali a.s. ni mbora wa Mawasii. Mawasii wangu baada yangu ni kumi na wawili. Wa kwanza wao ni Ali a.s. na wa mwisho wao ni Mahdi a.s." . Allah swt amesema katika Qur'an Tukufu , Sura al-Ahzab, 33 Ayah 33, 'Allah anataka kukuondoleeni uchafu, enyi watu wa Nyumba (ya Mtume ) na kukutakaseni kabisa kabisa.' . Allah swt amesema katika Qur'an Tukufu , Sura al-Ahzab, 33 Ayah 56, 'Hakika Allah na Malaika Wake wanamteremshia Rehema Mtume, basi enyi Waumini (Waislamu) msalieni Mtume na muombeeni Amani' . Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. katika Yanabiul Mawaddah, uk 42, 217 : "Mimi nawaachia nyinyi Makhalifa wawili; Kitabu cha Allah swt : ni kamba iliyonyoshwa kutoka mbinguni mpaka ardhini, na Jamaa zangu wa Nyumba yangu (Ahlul-Bait a.s.)"


. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. katika Yanabiul Mawaddah, uk 30/31 "Mfano wa Ahlul Bait zangu kwenu ni kama mfano wa jahazi ya Nuh a.s. , mwenye kupanda jahazi hiyo ameokoka na mwenye kuiachilia, kapotea." . Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. katika Sahih Muslim, Kitabu Al-Fadhail, mlango wa Fadhail Ali a.s. kwa kiingereza ni : J.4, uk. 1286, Hadith nambari 5920 : "….Enyi watu ! …. Ninawaachia nyinyi vizito viwili : Cha kwanza ni Kitabu cha Allah swt chenye uongozi na mwangaza basi shikamaneni na Kitabu cha Allah swt …. Na watu wa Nyumba yangu (Ahlul Bait a.s. )"


. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. Musnad Bin Hanbal, j. 4; uk. 437 : "Hakika Ali ni kiongozi wa kila Mumiin baada yangu." . Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. katika At-Tirmidhi, j.5, uk. 66 Na.3786 "Enyi Watu ! Mimi hakika nimekuacheni vitu viwili navyo ni Kitabu cha Allah swt (Qur'an ) na watu wa ukoo wa Nyumba yangu (Ahlul-Bait a.s.). Mkivichika viwili hivyo milele hamtapotea."

. Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema "Mkipata neema chache msirudishe kwa uchache wa shukurani." . Allah swt amesema katika Qur'an Tukuf, Sura Al-Imran, 3, Ayah 179 : 'Wala usidhani wale waliouawa katika njia ya Allah swt kuwa ni wafu, bali wahai wanaruzukiwa kwa Mola wao.' . Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema : "Changanyikeni na watu kiasi ambacho kama mkifa watawalilia na mkiishi watatamani kuwa nanyi."


. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. katika Al-Ghadiir : "Siku ya Ghadiir Khum ni Idi bora mno kwa Ummah wangu." . Allah swt amesema katika Qur'an Tukufu, Surah…, …., Ayah…., 'Shikamaneni na kamba ya Allah na wala msifarakane.'

SEMI MCHANGANYIKO
. "Uwe mpole na mwenye huruma kwa wale walioko chini yako au amri yako." . "Uchukue tahadhari na wala usidanganyike na ving'aavyo." . "Umwie ndugu yako kwa uwema hata kama ametokezea kwako kukudhuru. Yeye anapo puuzia au kuukanusha udugu nawe, umwijie kindugu, utokezee awapo katika shida na ujaribu sana ili uweze kumsaidia katika hali hiyo. Awapo mchoyo au bahili kwako na akupuuzapo pale uwapo na mahitaji ya msaada wa kifedha, uwe mkarimu na umsaidie kifedha kwa kiasi uwezacho. Iwapo yeye ni mjuvi na mkatili kwako, basi wewe uwe mpole na umhali yeye. Iwapo anakudhuru, uyakubalie hoja zake. Uishi nae kama kwamba wewe ni mfaidika. Lakini uwe mwangalifu sana kuwa wewe usiwe hivyo kwa wasio stahiki na walio waovu.

. "Usiimarishe urafiki na maadui wa marafiki wako kwani na rafiki yako atakugeuka wewe na kujitokezea mbele yako kama adui pia." . "Umshauri na kumpatia mawaidha mema na bora sana rafiki yako hata kama yeye hatapendelea hivyo." . "Uimarishe vyema na kusawazisha hasira, kwa sababu mimi sijawahi kuona faida yoyote ile iliyo zaidi kuliko kujizuia hivyo." . "Usimkorofishe mtu ambaye akufikiriaye wewe kuwa u mzuri na mwema na wala usijaribu kumfanya ajaribu kukugeuka.


. "Usiwe mbaya kwa watu wa nyumbani mwako (mke, watoto na wakutegemeao) na wala usiwe kwao kwa ghadhabu na mkatili yungali hai." . "Usimkimbilie yule akupuuzaye." . "Kamwe usiwaijie kwa ubaya wale waliokufanyia hisani." . "Masikini ni yule ambaye hana marafiki. Yeyote yule akunashaye haki na kujiona kuwa maisha yake yanamzonga na zenye kumtatanisha basi ni mtatanishi." . "Uhasiano ulio bora kabisa ni ule kati ya mtu na Allah swt.". "Uahirishe matendo yako maovu kwa kipindi kirefu kwani wewe unaweza kuyatenda popote pale utakapo penda (kwa hivyo kwa nini uwe na haraka ya kutenda?)" . "Uchukue mambo mema kutoka kila tawi la elime kama vile nyuki atafutavyo asali (utamutamu) kutoka kila ua zuri. . "Kumbuka kwa chochote kile kilivyo kidogo ambacho umepatiwa na Allah swt kitakuwa ni chenye manufaa zaidi na huduma zaidi kwako na ni yenye heshima kwa uwingi usio na maana. Uelewe vyema kuwa kiasi chochote kile mtu mwingine atakacho kukupatia ni sehemu mojawapo ya kiasi alichomjaalia Allah swt ." . "Hasara uipatayo wewe kutokana na ukimya wako unaweza kufidiwa kwa urahisi, lakini hasara itakayotokana na kusema kupita kiasi na kusema ovyo itakuwa vigumu kuyarudia. Je hauoni kuwa njia iliyo bora ya kuyalinda maji katika bwawa ni kwa kuufunga mdomo wake ?"


. "Kulinda na kuhifadhi kile ulichonacho na kilicho chako ni afadhali kuliko kuomba na kutamani vile walivyonavyo wengine." . "Marejeo yatokanayo na kazi za mikono au uhodari wa ufundi kwa njia ya heshima na utukufu ingawaje hata kama ikiwa ni kidogo, ni heri ya utajiri ambao wewe unaweza kuupata/kuulimbika kwa kufanya madhambi maovu." . "Hakuna mhifadhi bora wa siri zako kuliko wewe mwenyewe." . "Kwa mara nyingi mtu anajaribu kila njia kujipatia kitu ambacho ndicho chenye kumletea madhara yeye. Na mara nyingi mtu hujitakia mabaya ya madhara mwenyewe."


. "Yule aliyenatabia ya kusema sana, ndiye afanyaye makosa mengi." . "Yule ambaye huwa na tabia ya kufikiri na kuyadhatiti mambo, huendeleza nguvu zake za kina na fikara na nuru ya macho." . "Riziki inayopatikana kwa njia isiyo halali ni njia ovu kabisa ya kupata riziki." . "Kwa kujijumuisha pamoja na awatu wema, wewe utaendeleza uwem katika tabia yako na kwa kujiepusha na makundi ya waovu, basi uwema ilivyo bora."


. "Iwapo huruma au upole wako utatokezea kutendwa kwa ukatili na uonevu basi ukomeshaji na kutilia mkazo mkali ndiyo huruma na uwema ilivyo bora." . "Kamwe usitumainie uzushi kwani ndizo rasilimali za wajinga au wapumbavu." . "Busara ndilo jina la mkondo wa kukumbuka uzoefu na kuitumia. Uzoefu uliyo bora zaidi ni ule ambao ukupatiao tahadhari iliyo bora na mawaidha yaliyo bora."


. "Kila mmoja ajaribuaye siye ndiye afanikiwae." . "Yeyote yule atakaeiaga (kufa) hii dunia, basi ajue kuwa hatarudipo tena." . "Karibuni utakipata kile alichokuidhinishia Allah swt kwa ajili yako."


. Allah swt Amesema katika Qur'an Tukufu, Surah Az-Zumar, 39 , Ayah 13 - 15 : "Mimi naogopa adhabu ya siku kama nikimuasi Mola wangu. Sema: "Namuabudu Allah swt kwa kumuitikadi kuwa yeye tu ndiye Allah swt ." "Basi nyinyi abuduni mnachopenda kisichokuwa yeye." (khiari yenu, lakini Allah swt atakulipeni tu); Sema: "Hakika watakao pata hasara ni wale walizotia hasarani nafsi zao na watu wao siku ya Qiyama. Angalieni! Hiyo ndiyo hasara iliyo dhahiri."


FADHAIL ZA IMAM ALI a.s.
. Kutokea 'Ala, amesema yeye: "Mimi nilimwuliza 'Aysha kuhusu 'Ali ibn Abi Talib. Mimi nilimwuliza Mtume s.a.w.w. kuhusu yeye. 'Ayesha alijibu, naye akasema kuwa 'Ali ni mtu bora kabisa katika Wanadamu, na hakuna mwenye shaka yoyote ile isipokuwa ni mpagani tu. . Na kutoka 'Ali ibn Abi Talib a.s., kasema: "Aliniambia Mtume Muhammad s.a.w.w. 'Wewe ni bora wa viumbe vya Allah swt, na hakuna mwenye shaka yoyote ile isipokuwa atakuwa ni kafiri' . Na kutoka kwa Hudhaifa: "Alisema Mtume Muhammad s.a.w.w. kuwa ' 'Ali ni bora wa Wanaadamu. Yeyote yule anayekataa haya kwa hakika ni kafiri.'


. Kutokea kwa Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. alisema: "Alisema Mtume Muhammad s.a.w.w. , 'uadui, chuki na bughudha dhidi ya 'Ali ibn Abi Talib ni ukafiri na uadui dhidi ya Bani Hashim ni unafiki.'" . Na kutokea kwake, kutokea Mtume Muhammad s.a.w.w. akasema: " Hakuna ampendaye 'Ali ibn Abi Talib a.s. isipokuwa ni mumiin halisi, na hakuna amchukiaye 'Ali isipokuwa ni kafiri."

. Na kutokea Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. , alisema: "Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. kuwa yeyote yule atakaye msema vibaya 'Ali ibn Abi Talib, basi ajue kuwa amenisema mimi vibaya hivyo, na yeyote yule anisemaye mimi vibaya, basi amemsema hivyo Allah swt (na hilo ni dhambi kuu )." . Amesema Al-Imam Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema: "Kwa hakika Allah swt alitazama kuelekea dunia hii na akanichagua mimi kutoka watu wa dunia; na kwa mara nyingine tena aliangalia duniani na kukuchagua wewe kutoka watu wa dunia; na kwa mara ya tatu alipoangalia akawachagua Maimamu a.s. kutokea vizazi vyako miongoni mwa watu wote wa dunia hii; na kwa mara ya nne alipoangalia akamchagua binti yangu Fatimah kutokea wanawake wote wa dunia hii."


. Kutokea Ja'abir, anasema kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema: " Ali ibn Abi Talib a.s. ni bora miongoni mwa watu wa dunia. Yeyote yule aliye na shaka, basi ni kafiri." . Amesema Ibn 'Abbas kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema: " 'Ali ibn Abi Talib a.s. ni mlango wa Hitta Yeyote yule atakayeingia ndani mwake basi kwa hakika ndiye mumiin wa kweli, na yeyote atakayetoka kutoka humo ni kafiri." . Al-Imam Muhammad al-Baquir a.s. kutokea baba yake amesema kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. aliulizwa kuhusu hali ya watu, naye akajibu " bora kabisa na Mcha Mungu halisi na ambaye aliye karibu kabisa nao ambay yuko karibu nami ni Ali ibn Abi Talib a.s. , na hakuna Mcha-Mungu halisi miongoni mwenu, na ambaye yupo karibu nami kuliko Ali ibn Abi Talib a.s."


. Jami' bin 'Omair, alisema kuwa yeye alimwuliza 'Ayesha kuhusu daraja la 'Ali ibn Abi Talib a.s. mbele ya Mtume Muhammad s.a.w.w. ? Yeye alijibu: " Kwa hakika ni mtu mwenye kuheshimiwa mno mbele ya Mtume Muhammad s.a.w.w." Yeye alimwuliza tena kuhusu nafasi ya Ali ibn Abi Talib a.s. katika macho ya Mtume Muhammad s.a.w.w. . Alijibiwa kuwa "Ni mtu mwenye kuheshimiwa mno mbele ya Mtume Muhammad s.a.w.w. ."

. Na kutokea Ibn 'Umar amesema kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema : "Bora wa mtu miongoni mwenu ni 'Ali ibn Abi Talib a.s. na bora wa vijana wenu ni Al - Hassan na Al -Husayn . 'Urwah anaripoti kutoka 'Ayesha kuwa: Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. "Kwa hakika nimeahidiwa na Allah swt kuwa yeyote yule atakayeinuka dhidi ya 'Ali ibn Abi Talib a.s. basi kwa hakika ni kafiri na kwa hakika ataingia Jahannam aunguzwe na moto. 'Aisha akasema kuwa "Mimi niliisahau hadith hii siku ya (vita vya) Jamal, hadi hapo nilipoikumbuka au nilipokumbushwa tukiwa Basra (Iraq), nami namwomba Allah swt anisamehe, na sitegemei kuwa miongoni mwao." . Abu Salim bin Abu al-Jaada amesema kuwa yeye alimwomba Ja'abir azungumze chochote kuhusu 'Ali ibn Abi Talib a.s. . Ja'abir kasema: "'Ali ibn Abi Talib a.s. alikuwa bora miongoni mwa wanadamu." Mimi nilimwuliza tena "Je unasemaje kuhusu mtu atakayemchukia 'Ali ibn Abi Talib a.s." Yeye alinijibu: "Hakuna atakayemchukia 'Ali ibn Abi Talib a.s. isipokuwa kafiri."


. Hashim bin Barid alisema kuwa 'Abdullah ibn Mas'ud alisema : "Mimi nilijifunza Sura 70 za Qur'an Tukufu kutokea kinywani mwa Mtume Muhammad s.a.w.w. na Surah za Qur'an zilizobakia nilijifunza kutokea mbora wa Ummah wetu yaani Ali ibn Abi Talib a.s." . Muhammad bin Salim al-Bazzar anasema kuwa yeye alikuwa pamoja na Said bin al-Musayyib katika Masjid-i-Nabi, siku ya Ijumaa, ndipo alipotokezea mhubiri kutoka kabila la Banu Omayyah (laana za Allah swt ziwafikie juu yao ) na akapanda juu ya mimbar na akaanza kumtusi Ali ibn Abi Talib a.s. kwa kusema: "Kwa hakika, Allah swt hakumtukuza Ali ibn Abi Talib a.s. kwa mapenzi yake ba dala yake amefanya hivyo kwa kuhofu uchochezi wake." Kwa hayo Said bin Al-Musayyib alimlaani na kumwambia: "Kwa hakika wewe unasema uongo mtupu" Na hapo alimtupia nguo aliyokuwa akijifunika juu ya mdomo wa mhubiri huyo. Hapo watu walipomwambia kuwa itakuwaje iwapo Abu Muhammad wakati Imam huyo anatokana na Banu Omayyah ? Hapo Said alijibu: "Kwa kiapo cha Allah swt ! Mimi sijui nilichokisema, lakini mimi nilimsikia Mtume Muhammad s.a.w.w. akisema haya kutokea makbara haya nami ndipo nilipoyarudia kuyasema."


. Ummi Hani binti Abu Talib a.s. kasema kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. kasema kuwa: "Bora wa viumbe vya Allah swt katika mtazamo wake Allah swt, ni yule anayelala kaburini mwake na kamwe hakumshuku 'Ali ibn Abi Talib a.s. na kizazi chake ni bora wa vizazi katika viumbe vyote." . Ja'abir anasema kuwa "Hakuna anayeshuku fadhail za 'Ali ibn Abi Talib a.s. isipokuwa ni kafiri na kasema kuwa "Kwa kiapo cha Allah swt sisi kamwe tulikuwa hatuwajui wanafiki, katika zama za Mtume Muhammad s.a.w.w. isipokuwa kwa yule mwenye chuki dhidi ya 'Ali ibn Abi Talib a.s."


. Said bin Ja'abir alise kuwa yeye alikuwa akimwongoza Ibn 'Abbas baada ya yeye kupoteza nuru ya macho yake, kutokea Msikitini, na aliwapita kundi la watu waliokuwa wakimtukana 'Ali ibn Abi Talib a.s. na aliniambia kuwa nimchukue hapo. Hivyo mimi nilimfikisha kwao. Kufika hapo alisema "Ni nani miongoni mwenu anayemkashifu Allah swt ?! Kwa hakika yeyote yule anayemkashifu Allah swt amekuwa kafiri. Na ni yupi yule anayemkashifu 'Ali ibn Abi Talib a.s. ? Na kwa hakika hili limetokea" akasema. Ndipo alipoendelea kusema: "Nashuhudia Allah swt, kwa kiapo cha Allah swt, mimi nilimsikia Mtume Muhammad s.a.w.w. akisema 'Yeyote yule anayemkashifu 'Ali ibn Abi Talib a.s. basi amenikashifu mimi na kwa hakika anayenikashifu mimi basi ajue kuwa amemkashifu Allah swt na yule anayemkashifu Allah swt, Mtume wake basi watatakiwa kutoa maelezo yake." Na hapo ndipo Ibn 'Abbas aligeuka.


. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. : "Muzirembeshe vikao vyenu kwa mazungumzo na makumbusho ya 'Ali ibn Abi Talib a.s. kwa dhikr ya ni dhikr zangu na dhikr zangu ndizo dhikr za Allah swt na dhikr za Allah swt ni 'ibadah. Na mwenye kufanya 'ibadah huingia Peponi."