HADITHI ZA MTUME (S.A.W.W)PAMOJA NA MAIMAMU (A.S)

 
. Muhammad bin Ali bin Hussein katika kitabu cha Amali amenakili riwaya kutoka Abul Ja'rud Ma'rifat kuwa Al Imam Muhammad al-Baquir a.s. amenakiliwa riwaya kuwa amezungumzia kuhusu ayah Qur'an Tukufu, Surah Al Maida, 5, Ayah 55: Hakika rafiki yenu mlinzi ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini, ambao hushika Sala na hutoa Zaka nao wananyenyekea kama ifuatavyo: "Katika Mayahudi ambaye mnafiki mmoja alipoukubalia Uislam akaanza kuiga: "Ewe Mtume wa Allah swt! Je ni nani Wasii na Khalifa wako? Na nani huyo atakaye kuwa Walii baada yako?"


Ndipo hapo ayah hiyo ilipoteremshwa na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akawaambia inukeni, basi hao wote wakainuka na wakaanza kuelekea msikitini. Walipofika msikitini wakakutana na maskini mmoja akitoka nje na hivyo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akamwuuliza, "Je kuna mtu yeyote aliyekupa chochote ?" Huyo akasema "Kwa nini isiwe hivyo pete hii je niliyoipata?" Kwa hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akasema,"Je ni nani aliyekupa?" Huyo mwombaji akasema "Huyo mtu ambaye bado anasali." Kwa hayo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akasema "Je alipokupa hiyo pete alikuwa katika hali gani?"


Huyo mwombaji akasema alikuwa katika hali ya Ruku'u. Na hapo ndipo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipopaaza sauti ya Takbira yaani Allahu Akbar na wale wote waliokuwepo pamoja naye nao pia walitoa Takbira kwa nguvu na sauti na hapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ndipo alipowaambia wote: "Mtambue wazi kuwa baada yangu Walii ni huyu Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. na wa si mwingine" Karta anasema kuwa "Kwa mujibu wa riwaya zilizopatikana kuwa katika sala moja aliitoa Hullah, na katika sala ya pili alitoa pete basi inadhihirika kuwa Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. anatoa sadaka katika hali ya sala zaidi ya mara moja ndivyo inavyothibitika kwa mujibu wa riwaya zinazopatikana."


. Ayyashi katika Tafsir yake ananakili riwaya moja kutokea kwa mwana wa Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. kwa Ammar Yasir amesema: "Siku moja Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. alipokuwa akisali sala ya Sunnah aliahirisha tendo moja kiasi kwamba mpaka akavua pete yake kwa ajili ya kumpa aliyekuja kuomba. Na pale Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipokuja basi alimwelezea hivyo. Na wakati huwo iliteremshwaayah yake hadi kufikia : Qur'an Tukufu, Surah Al Maida, 5, Ayah 55: Hakika rafiki yenu mlinzi ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini, ambao hushika Sala na hutoa Zaka nao wananyenyekea Basi Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alitusomea ayah hiyo na akasema,


"Yeyote yule ambaye mimi ni Mawla wake basi Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. ni Mawla wake. Ewe Allah swt! Uwe na mapenzi na yule ambaye anawapenda wao, na uwe na uadui na yule ambaye anafanya uadui pamoja nao." . Halabi anasema kuwa yeye alipomwuliza Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. basi Imam a.s. akamjibu: "Naam kabisa! Al Imam Hassan ibn 'Ali ibn Abi Talib a.s. aligawa nusu ya mali yake katika njia ya Allah swt - hadi kwamba nguo kwa nguo, Dinar kwa Dinar, alivigawa vyote katika njia ya Allah swt, na alikwenda Hija ishirini kwa kutembea na miguu."


. Mtume Muhammad s.a.w.w. Amesema, Wasa'il ush-Shi'ah, J. 6, Uk. 13: "Umma wangu utaendelea kuishi kwa heri pale watapokuwa waaminifu miongoni mwao, watakapokuwa wakirejesha amana watakazokuwa wakiachiana, na watakapokuwa wakitoa sadaka kutoka mali zao; Lakini, Iwapo wao hawatatimiza wajibu hizo, basi watakumbwa na ukame na baa la njaa."


. Amesema Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s., Nahjul Balagha, uk.512, Msemo 254 : "Enyi wana wa Adam ! Muwe wawakilishi wenu wenyewe katika mali yenu na mfanye kile chochote kile mnachotaka kufanyiwa nyie baada ya kifo chenu." Tanbih Iwapo mtu atataka baada ya kifo chake sehemu fulani ya mali utajir wake utumike katika kutoa sadaka au misaada, basi asisubiri mpaka afe bali aitumie popote pale atakapo katika uhai wake kwa sababu inawezekana kuwa baada ya kifo chake warithi wake wasiweze kutekeleza kwa mujibu wa vile alivyotaka au usia wake na labda inawezekana asipate wakati wa kuandika usia hivyo akakosa fursa hiyo."


. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema, Kanz-ul- 'Ummal, J. 6, Uk. 371: "Toeni sadaka na muwatibu wagonjwa wenu kwa hayo, kwa sababu sadaka kwa hakika inatoa balaa na magonjwa; na inaongezea umri wenu ukawa mrefu na kuongezeka kwa thawabu zenu."

. Imenakiliwa kutoka Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akisema, Al-Ithna-'Asheriyyah, Uk. 85: "Nilipokuwa nimekwenda mbinguni, mimi niliona mistari mitatu imeandikwa juu ya mlango wa Jannat: Mstari wa kwanza ulikuwa umeandikwa Bismillah Rahman Rahim; Mimi ni Allah swt na hakuna Allah swt mwingine isipokuwa mimi na Rehema zangu zinazidi adhabu zangu. Mstari wa pili ulikuwa umeandikwa Bismillah Rahman Rahim; Sadaka inalipwa kwa mara kumi (10) na mkopo unalipwa mara kumi na nane (18), na kuwajali maJama'a na ndugu kunalipwa mara thelathini (30). Mstari wa tatu ulisomwa yeyote yule anayeelewa wadhifa Wangu na Ukuu wangu basi kamwe asinishutumu mimi katika maswala ya maisha."


. Taus-ibn-il-Yamani anasema kuwa yeye alimsikia Al Imam Zaynul 'Abediin a.s. akisema sifa za muumin ni tano na pale alipoombwa kuzitaja alijibu, Khisal-i-Sadduq, Uk. 127: "Ucha Allah swt katika hali ya upweke, kutoa sadaka wakati unaohitajika, Subira anapopatwa na matatizo au anapokuwa na shida, uvumilivu wakati wa ghadhabu, ukweli ponapokuwa na hofu."


KUTOA SADAKA NA UBAHILI:
. Mali ya mchoyo huliwa na warithi wake au hupeperuka bila
kujulikana.
. Hakuna mtu mwenye upweke vile alivyo bahili.
. Mchoyo ni mweka/mtunzi hazina wa warithi wake.
. Ubahili na uchoyo huangamiza upendo wa urafiki wa kweli.
. Ubahilifu ni kujipatia ubadhirifu.
. Kuwa mchoyo kwa kile ulichonacho ni kutomwamini Allah swt.
. Sifa ya upole na wema huangamizwa kwa ubahili.
. Fedha haimnufaishi mwenye kuwa nayo hadi hapo atenganapo nayo.
. Maovu hufichwa kwa ukarimu.
. Bora wa watu ni yule afaaye watu
. Hakutakuwa kuwafadhili watu kwa mifuko mitupu.
. Fadhila huuliwa kwa matumizi fidhuli.
. Uachie ngome ya Sadaqa iilinde ufanisi wako.
. Kutoa baada ya kughairi ni bora zaidi kuliko kughairi baada ya kutoa.
. Uso ulio mcheshi ni mojawapo ya ne'ema mbili.
. Usimuudhi mtu yeyote yule pale akutakiapo kila la kheri.
. Fadhila na ukarimu hupatiwa sifa.
. Fadhila ya kweli (kwa moyo safi) huondoa dhiki zote
. Makosa ya mwenye kutoa fadhila ni afadhali kuliko dharau ya mchoyo.
. Fadhila isiongozwe kwa uoga wala kuwa na matumainio ya kupata chochote (tamaa).KUWAJALI NDUGU NA MAJAMA'A.
. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema, Bihar al-Anwaar, J. 74, Uk. 89: "Yeyote yule anayetaka kuongezewa riziki na baraka na siku yake ya mauti icheleweshwa, basi inambidi awajali ndugu na maJama'a zake." . Amesema Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s., Bihar al-Anwaar, J. 73, Uk. 138: "Mali haiwezi kulimbikana kupita kiasi isipokuwa kwa njia tano: Ubahili kupita kiasi, matarajio makubwa sana, uroho kupita kiasi, kuvunja uhusiano pamoja na ndugu na maJama'a za mtu mwenyewe, na kuijali na kuipenda dunia hii kuliko Akhera."


. Al Imam Muhammad al-Baquir a.s. Amesema, Al-Usul-i- Kafi , J. 2, Uk. 150: "Kuwajali Jama'a na ndugu kunaleta faida tano: Kutakasika na kukubalika kwa matendo ya mtu Kuongezeka katika utajiri na mali Kuondoa balaa na shida mbalimbali Kurahisisha maswala yake katika Akhera Umri kuwa mrefu." . Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema, Al-Khisal Uk. 179: "Kuna makundi matatu ya watu ambao hawataruhusiwa kuingia Jannat: Wanywaji wa pombe, Wachawi , na wale wanaokana Jama'a na ndugu zao.


KUWAHURUMIA WAZAZI.
. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Mustadrak Al-Wasa'il-ush-Shiah, J. 15, Uk. 176: "Furaha ya Allah swt ipo katika furaha ya wazazi wa mtu (kama ndio hivyo ni kweli, basi adhabu na ghadhabu zake pia zipo katika ghadhabu za wazazi wa mtu)." . Amesema Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s., Bihar al-Anwaar, J. 74, Uk. 85: "Bora ya matendo ni: Kusali kwa wakati wake, kuwa mwema na mwenye huruma na mwenye mapenzi kwa wazazi wake, na kuchangia katika vita vitakatifu vya Jihad (dhidi ya Mapagani) katika njia ya Allah swt."


. Amesema Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s., Safinat-ul-Bihar, J. 2, Uk. 553: "Iwapo mtu anataka Allah swt ampunguzie makali ya mauti, basi lazima awajali Jama'a na ndugu zake, na awawie wema wazazi wake. Na pale mtu anapofanya hivyo, basi Allah swt atampunguzia makali ya mauti na kamwe hatapata umaskini katika maisha yake." . Amesema Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s., Al-Usul-i- Kafi, J. 2, Uk. 349: "Yeyote yule anayewatazama wazazi wake kwa macho ya ghadhabu, hata kama wao hawakuwa waadilifu kwake, basi Allah swt hatazikubalia ibada za mtu huyo (hadi hapo atakapofanya Tawba)." . Amesema Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s., Al-Kafi J. 5, Uk. 554: "Watendee wazazi wako kwa huruma ili na watoto wako waje wakutendee vivyo hivyo; na uwe mcha Allah swt kwa wake wa watu wengine ili wake zako wabakie wacha Allah swt."


. Amesema Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s., Al-Kafi J. 2, Uk. 162: "Safari moja mtu alimwijia Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na kumwuliza namna ya kuwashughulikia wazazi. Hapo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimjibu uwe mwenye huruma kwa mama yako: uwe mwenye huruma kwa mama yako na uwe mwenye huruma kwa mama yako; Uwe mwenye huruma kwa baba yako uwe mwenye huruma kwa baba yako; na uwe mwenye huruma kwa baba yako lakini huruma hiyo uianzie kwa mama yako kabla ya baba yako."


HAKI ZA WATOTO.
. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwambia Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s., Wasa'il ush-Shi'ah, J. 31, Uk. 290: "Ewe Ali ! Allah swt huwalaani wazazi wale wanao wafanya watoto wao wasiwe watiifu kwao kwa sababu ya kuwalaani kwao." . Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. alimwambia mmoja ya wafuasi wake, Nahjul Balagha Uk. 536, Msemo, No. 352: "Usiupitishe wakati wakati wako mwingi pamoja na mke wako na watoto wako waliokuwa wakubwa, kwa sababu kama mke wako na watoto wako ni wampendao Allah swt, basi Allah swt hatawaacha wapenzi wake bila ya kuwajali, iwapo watakuwa ni maadui wa Allah swt, basi kwa nini wewe uwe na wasiwasi na ujiweke mashughuli kwa ajili ya maadui wa Allah swt.


Na mambo mawili yanayoweza kuchukuliwa katika wanaume katika kuhusiana na kuwapatiapo familia zao. Moja ni kutokutimiza wajibu wake kwao, na pili kinachotajwa hapa ni kulimbikiza kupita kiasi kwa mali kwa ajili yao." . Amesema Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s., Al-Kafi J. 6, Uk. 47: "Chukueni hatua za kuwafundisha watoto wenu riwaya na ahadith za Ahlul Bayt a.s. kabla watoto wenu hawajaharibika na hawajachafuliwa akili zao." . Amesema Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s., Man la Yahdharul Faqih, J. 3, Uk. 483: "Heri ya mtu kwa mtoto wake ni kule kwa mtoto wake kuwa heri kwa wazazi wake."


. Amesema Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s., Nahjul Balagha, Msemo 399: "Haki ya mtoto kwa wazazi wake ni kwamba apewe jina zuri kabisa, afundishwe adabu njema na afundishwe Qur'an kwa kanuni zake." . Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Al-Kafi J. 6, Uk. 47: "Wafundisheni watoto wenu kuogelea na kulenga shabaha." . Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Kanz-ul- 'Ummal, J. 16, No. 45, 330: "Watoto wenu wanapokua kufikia umri wa miaka saba, wafundisheni sala, wanapokuwa na umri wa miaka kumi, muwalazimishe kusimamisha sala; na mutenganishe vitanda vyao vya kulalia."


. Amesema Al Imam Zaynul 'Abediin a.s. : Man la Yahdharul Faqih, J. 2, Uk. 622: "Haki ya mtoto wako ni kwamba wewe utambue wazi kuwa yeye amekuja humu duniani kwa kukupitia wewe, kwa hiyo yaliyo sahihi na yaliyo mabaya yanatokana na wewe. Wewe unawajibika kumpa mafunzo na elimu bora, kumwelekeza kwa Allah swt, na kumsaidia katika kumtii Allah swt. Kwa hivyo iwapo utamsaidia utamfanyia hisani mtoto wako, basi utaweza kufikia malengo hayo; na kama wewe utamwia kiovu, basi hayo yatakurejea wewe mwenyewe." . Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema, Bihar al- Anwaar, J. 104, Uk. 95: "Muwaheshimu watoto wenu na muwafundishe kuwa wema, mtasamehewa na Allah swt."


KUNYOYESHA MAZIWA
. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Man la Yahdharul Faqih, J. 3, Uk. 561: "Naam malipo ya mwanamke wakati wa mimba yake hadi kuzaa mtoto, na wakati pale anapolea mtoto ni sawa na kuwekwa askari katika kituo cha kulinda mipaka ya Waislam dhidi ya hujuma za makafiri, kwa ajli ya Allah swt. Kwa hivyo iwapo atakufa katika kipindi hiki, basi mwanamke huyo atakuwa katika daraja la mashahidi." . Amesema Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s., Wasa'il ush-Shi'ah, J. 21, Uk. 452: "Hakuna maziwa yenye faida zaidi kwa mtoto isipokuwa maziwa anayonyonya kutoka kwa mama yake."


. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Bihar al- Anwaar, J. 104, Uk. 106: "Wakati mwanamke anaposhika mimba basi atakuwa ni kama mpiganaji ambaye anafunga saumu wakati wa mchana na anakesha usiku kucha katika 'ibada, na amejitolea mhanga maisha yake na mali yake katika njia ya Allah swt. Hivyo anapozaa anapata malipo makubwa sana ambayo hakuna mtu anayeelewa isipokuwa Allah swt mwenyewe. Na pale anaponyonyesha mtoto maziwa basi atapata thawabu za kumfanya mtoto mmoja kuwa huru kutoka katika kizazi cha Mtume Ismail a.s. kwa kila mara atakapo nyonyesha. Na wakati ufikapo kipindi cha kumuachisha mtoto kunyonya, basi malaika aliyekaribu naye humwambia kuanza matendo kwa mara nyingine tena kwani kwa hakika yeye sasa hivi alipo ni katika hali ya kusamehewa kikamilifu (yaani ashike mimba na kuzaa na kunyonyesha tena kwa mara nyingine)."


. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema, Mustadrak- ul-Wasa'il, sehemu ya 48: "Hakuna maziwa yaliyo bora kabisa kwa mtoto isipokuwa maziwa ya mama yake." NDOA 'IBADA KUU. . Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema, Man la Yahdharul Faqih, J. 3, Uk. 384: "Raka'a mbili za sala zinazosaliwa na mtu aliyeoa ni nzito kuliko yule asiyeoa ambaye anakesha usiku kucha katika ibada na kufunga saumu nyakati za mchana." . Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Bihar al- Anwaar, J. 103, Uk. 221: "Usingizi wa mtu aliyeoa ni afadhali mbele ya Allah swt kuliko ibada afanyazo mtu asiyeoa usiku kucha na anayefunga saumu nyakati za mchana."


. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Bihar al- Anwaar, J. 103, Uk. 221: "Wengi wa watendao wema katika 'ummah wangu ni wale waliooa na kuolewa wakati watendao maovu wengi wao ni wale wasio oa au kuolewa." . Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anasema, Bihar al-Anwaar, J. 103, Uk. 217: "Siku moja mtu mmoja alimwijia baba yangu naye a.s. alimwuliza iwapo alikuwa ana mke naye akajibu alikuwa hana. Hapo baba yangu a.s. alimjibu kuwa yeye hawezi kulala usiku mmoja bila ya mwanamke hata kama atapewa badala yake dunia nzima na yale yote yaliyomo ndani yake. Na hapo Imam a.s. alimwambia kuwa Raka'a mbili anazosali mtu aliyeoa ni bora kuliko ibada ya yule asiyeoa kwa kukesha usiku kucha na kufunga saumu katika nyakati za mchana. Na baadaye Imam a.s. alimpa Dinar za dhahabu saba na akamwambia akaolee kwa hayo."


KUWAPA HIMA KWA AJILI YA KUOA.
. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema, Al-Kafi J. 5, Uk. 328 : "Mtu anayeoa hujipatia nusu ya imani yake, na nusu ya imani inayobakia lazima awe na Taqwa." . Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema: Man la Yahdharul Faqih, J. 3, Uk. 384: "Wengi wa watu wa Jahannam watakuwa wale wasioolewa (bila kujali mwanamme au mwanamke)."


. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., At-Tahdhib, J. 7, Uk. 239: "Wengi wa wapotofu na walio haribika katika wale walio kufa miongoni mwenu ni wale wasioolewa na wasiooa." . Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Man la Yahdharul Faqih, J. 3, Uk. 385: "Yeyote yule anayetaka awe msafi na aliye takasika wakati atakapo onana na Allah swt, basi aoe na awe na mke."

. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. : Bihar al- Anwaar, J. 103, Uk. 221: "Oeni, ama sivyo mtahesabiwa miongoni mwa Rahbani au ndugu wa maShaytani."

NDOA NI UFUNGUO WA REHEMA ZA ALLAH SWT NA BASHARA NJEMA.
. Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Bihar al- Anwaar, J. 103, Uk. 221: "Milango ya Jannat kwa rehema itafunguliwa katika nyakati nne: Pale inaponyesha mvua, wakati mtoto anapoangalia kwa huruma nyuso za wazazi wake, pale wakati mlango wa Al Ka'aba tukufu inapofunguliwa, na pale ndoa inapofanyika."


. Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema: Bihar al- Anwaar, J. 103, Uk. 222: "Waunganisheni watoto wenu wavulana kwa wasichana kwa ndoa kwa sababu, humo Allah swt huwajaalia tabia njema, na huwazidishia katika riziki na heshima zao." . Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Amesema, Al-Kafi J. 5, Uk. 328: "Muolewe na muwaoze mabinti zenu, kwa sababu ni bahati nzuri kwa Mwislamu mwanamme kumtoa au kuwapa mtoto wake aliyekua au dada yake kwa ajili ya ndoa." . Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w., Al-Kafi J. 5, Uk. 328: "Hakuna kilicho kipenzi mbele ya Allah swt kuliko ile nyumba ambayo kuna maamrisho ya Islam yanatekelezwa kwa ndoa; na hakuna kitu chochote kinacho mghadhabisha Allah swt kuliko nyumba ile ambamo kunatokea talaka na ufarakano na utengano kati ya bibi na bwana."