HADITHI ZA MTUME (S.A.W.W)PAMOJA NA MAIMAMU (A.S)

 
. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa Ayah ya Qur'an Surah Al-Hajj, 22, Ayah ya 28: Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalumu juu ya nyama hoa alio waruzuku. Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri. "Allah swt katika ayah hii anamaanisha kuwalisha wale walio na shida na kuwasaidia, ambapo wao kwa heshima zao wenyewe hawajitokezi nje mbele ya watu kuomba." . Isack bin Ammar amenakili riwaya kutoka Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa: "Utafika wakati mmoja ambapo waombaji wanaorefusha mikono yao kwa watu watakuwa wakiishi kwa starehe na wale watakao kaa kimya kwa kutunza heshima zao watakuwa wakifa kwa shida zitakazo kuwa zikiwakabili.


Kwa hayo mimi nikamwuliza Imam a.s., "Ewe Maula ! Je yakitokea hayo katika zama za uhai wangu mimi nifanyeje?" Kwa hayo Imam a.s akamjibu, "Kwa hakika kile ulichonacho wewe uwasaidie hao watu kwa hali na mali na kwa hata cheo chako ulicho nacho na kwa wadhifa wako ulio nao uwasaidie ipasavyo." . Abu Basir anasema kuwa Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. aliitolea maelezo Ayah ya Qur'an Tukufu Surah Al Baqara, 2, ayah ya 267 isemayo: Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa.


amesema Kuwa: "Zama kabla ya Islam watu walikuwa wamejilimbikizia mali iliyopatikana kwa njia zisizo halali (kwa njia zilizo haramu) na baada ya wao kusilimu, walikuwa wakidhani kuwa kwa kutoa mali iliyo patikana kwa njia haramu, watakuwa wametakasisha mali yao iliyo halali, kwa hivyo Allah swt alitoa amri kuwa sadaka itolewe kutoka mali iliyo halali tu." . Kwa kuzungumzia ayah hiyo ya juu Shahab amenakili riwaya kutoka Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa: "Ambamo amesema kulikuwa na kaumu moja ambayo walikuwa na mali nyingi iliyo chafu (iliyopatikana kwa njia za haramu ). Wakati wao walipoukubalia Islam walianza kuchukizwa na malimbikizo yao hayo machafu na wakataka kutoa kwa njia za sadaka. Allah swt aliwaonya kwa kuwaambia kuwa sadaka hutolewa kutokea mali iliyo halali tu." . Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema: "Iwapo watu watachuma au watajipatia mali kwa mujibu wa hukumu za Allah swt na wakaitumia kinyume na hukumu za Allah swt au iwapo watachuma kwa njia zilizo kinyume na hukumu za Allah swt na wakazitumia kwa mujibu wa hukumu za Allah swt; katika hali zote mbili Allah swt hazikubalii.


Katika kutaka kukubaliwa sharti ni kwamba mapato hayo yawe yamepatikana kwa njia zilizo halali na zitumiwe katika njia zilizo halali vile vile." . Halabi anasema kuwa mtu mmoja alimwuliza Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuhusiana na ayah hii katika Qur'an Tukufu Surah Al Baqarah, 2, ayah ya 267: Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa. Na hapo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akasema: "Wapo baadhi ya watu ambao baada ya kuingia katika Uislam bado wameendelea kubakia na mali iliyopatikana kwa njia zisizo halali. Na humo kulikuwa na mmoja ambaye kwa makusudi alianza kutoa sadaka kutoa mali hiyo isiyo halali. Na Allah swt alimzuia kufanya hivyo yaani sadaka haiwezi kutolewa isipokuwa kutokea mali iliyotokana kwa njia halali."


. Katika Ma'anil Akhbar Al Imam Hassan al-'Askari a.s. kwa kupitia sanad amenakili riwaya moja kutoka Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa amesema: "Wale ambao wanajiona utukufu na wakubwa na ambao wanatenda matendo kwa mujibu wa nafsi zao, mfano wake ni wa yule mtu ambaye mimi nilisikia watu wakimsifu sana na kumheshimu sana, na hivyo mimi nikawa na shauku ya kutaka kuonana na mtu huyo lakini katika hali ambayo yeye hataweza kunitambua. Siku moja mimi nilimwona alikuwa amezingirwa na watu. Baada ya muda mchache kupita mimi nikamwona yeye ametoka humo na akawa anaondoka, basi mimi nilimfuata nyuma yake.

b Tulipita katika duka la muuza mikate, huyo mtu kwa kuficha macho yake na kificho ficho akaiba mikate miwili. Kwa hakika mimi nilistaajabishwa mno, na nikadhani kuwa labda wao wana maelewano fulani kabla ya tukio hilo. Tukaendelea mbele yeye akamghafilisha mfanya biashara huyo na akaiba makomamanga mawili humo. Na hapa pia nikafikiria kwa labda wao watakuwa na maelewano kama hayo kabla ya kutokea tukio hili, nikiwa hapo nikaingiwa na wazo kuwa je iwapo watakuwa na maelewano kama hayo basi kwa nini achomoe vitu kimafichoficho? Basi mimi niliendelea kumfuata nyuma yake, tukafika njiani akamwona mtu mmoja mgonjwa basi huyo akasimama kwa mgonjwa huyo na akatoa ile mikate miwili na hayo makomamanga mawili, akampa huyo mgonjwa.
bb Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akamwuliza huyo mtu kulikuwa na dharura gani kwa kufanya hivyo. Mtu huyo kwa kuniona mimi akasema je wewe ni Ja'afar bin Muhammad ? Nami nikamjibu naam, basi yeye hapo akaanza kusema nasikitika sana kwa kutokujitambulisha kwako hapo kuja kukufikishia faida (kwa sababu Imam a.s. alikuwa hakujionyesha kuwa yeye ni Imam bali alikuwa amejiweka kama yeye ni mtu wa kawaida) Imam a.s. akamwambia kwa hakika matendo yako hayo yana aibisha. Basi yeye akasema kuwa Allah swt anasema katika Qur'an Tukufu Surah An A'Am, 6, Ayah 160: Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. Na afanyae ubaya hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa.


Ama kwa mujibu wa ayah ya Qur'an Tukufu mimi nimeiba mikate miwili hivyo nimetenda madhambi mawili na nimeiba makomamanga mawili hivyo nimetenda madhambi wawili na kwa ujumla nimetenda madhambi manne. Na pale mimi nilipompa mgonjwa sadaka mimi kwa kila wema nimepata malipo kumi ya thawabu hivyo jumla nimepata malipo ya thawabu arobaini. Na kutoka arobaini ukitoa nne ninayo mema thelathini na sita bado." Kwa hayo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akamjibu: "Mama yako akae kwenye kilio chako! Wewe kwa hakika umeitoa maana isivyo ya Ayah za Qur'an Tukufu. Je wewe huelewi ayah ya Qur'an Tukufu isemayo Surah Al Ma'ida, 5, Ayah ya 30:


Basi nafsi yake ikampelekea kumuuwa nduguye, akamuuwa na akawa miongoni mwa wenye kukhasirika. Kwa mujibu wa ayah hiyo wewe umeiba mikate miwili umetenda madhambi mawili na kwa kuiba makomamanga mawili umetenda madhambi mawili mengine na hivyo jumla umetenda madhambi manne, na pale ulipotoa hiyo mali yaani mikate na makomamanga, kama sadaka bila idhini ya mwenye mali basi umetenda madhambi mengine manne. Kwa hivyo umetenda madhambi nane kwa pamoja. Sasa wewe unafikiria mema hayo arobaini yametoka wapi?" Kwa hakika mtu huyo aliduwaa, akimwangalia Imam a.s. na akajiondokea zake. Baada ya hapo Imam a.s. akasema kwa kujitolea maana potofu ya ayah za Qur'an Tukufu vile isivyo sahihi ndio matokeo yake haya na vile vile kuwapotosha watu wengine pia."


. Katika tafsiri Ayyashi Al Imam Muhammad al-Baquir a.s. amenakiliwa akitoa tafsiri ya ayah Surah Al Baqara, 2, ayah ya 267: Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msinge vipokea ila ingekuwa mmefumba macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Msifiwa. Imam a.s. akaelezea: "Miongoni mwa watu kulikuwa kumelimbikwa mali iliyopatikana kwa riba na njia zingine zisizo za halali, basi wao walinuia kutoa sadaka humo, na ndipo Allah swt alipowakataza kufanya hivyo (kutoa sadaka kutoka mali iliyopatikana kwa njia za haramu hairuhusiwa)." . Al Imam Muhammad al-Baquir a.s. ameripoti riwaya kutoka kwa Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa amesema: "Katika vitu vya kuleta uokovu mojawapo ni kuwalisha chakula wale wenye kuwa na shida na dhiki, na pili mtu awe ni mwanzilishi awe ni mwanzo wa kutoa salamu na vile vile wakati watu wamelala usingizi mtu anaamka kwa ajili ya kusali na kufanya 'ibada."


b . Muhammad Yakub amenakili kutoka 'Ali bin Ibrahim ambaye naye amenakili kutoka Muhammad bin 'Isa bin 'Ubaid ambaye naye amenakili kutoka Ahmad bin Muhammad naye amenakili kutoka ibn Fazzal Ma'aruf naye kutokea Tha'alaba bin Maymun ambaye naye pia amenakili riwaya hiyo kutoka kwa Zararah, kuwa . Al Imam Muhammad al-Baquir a.s. amesema kuwa: "Allah swt hupendezewa mno kulishwa chakula wale wenye dhiki na shida na njaa, na vile vile hupendezewa kutolewa kwa dhabihu (qurbani)." . Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. amesema: "Yeyote yule ambaye hakubahatika kutufanyia sisi wema basi ni wajibu wake kuwafanyia mema na kuwatimizia mahitaji ya marafiki zetu. Na yeyote yule ambaye hakubahatika kudhuru makaburi yetu basi adhuru makaburi ya wafuasi na marafiki zetu."


. Muhammad bin Ali bin Hussein Jamil amenakili riwaya moja kutoka kwa Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa: "Miongoni mwenu mtu aliye bora kabisa ni yule mwenye moyo mkarimu yaani mwenye moyo wa kutoa na mtu mwovu kabisa ni yule ambaye ni bahili. Na usafi wa imani dalili yake ni kwamba huwawia kwa wema muumin wenzake na kuwatimizia dharura na mahitajio yao. Bila shaka yeyote yule anayewafanyia hisani ndugu zake katika imani basi ndiye mpenzi wa Allah swt kwa sababu katika kufanya wema huko kuna mambo mengi yanayomzuia mtu asiingie katika mitego ya Sheitani na vile vile asiingie Jahannam, na kwa matokeo yake ndiye mtu anayeingia Jannat." Baada ya hapo Imam a.s. alimwambia Jamil, "Ewe Jamil! Habari hizi uwafikishie wenzako. Kwa hayo mimi nikasema, "Ewe mwana wa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ! Niwe fidia juu yako. Je ni watu gani hao?" Imam a.s. akasema: "Hao ni wale ambao wanawafanyia wema ndugu zao katika imani wakati wa shida huwa pamoja nao na vile vile wakati wa furaha pia huwa nao."


. Sheikh Sadduq a.s. amenakili riwaya kutoka kwa Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ambaye amesema kuwa: "Yeyote yule ambaye hakupata fursa kufanya wema nasi, basi awafanyie wema wapenzi na wafuasi wetu basi atapata thawabu za kutufanyia wema sisi. Na vile vile ambaye hakubahatika kutuzuru sisi katika uhai wetu na uhai wake basi awazuru wapenzi na wafuasi wetu, basi atapata thawabu kama za kutuzuru sisi." . Safwan Al-Jammal anasema kuwa siku moja Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. alimwambia Mu'alla bin Hunais: "Ewe Mu'alla! Uwe wa Allah swt, ili Allah swt aweze kukutunza na kukuhifadhi. Kwa hayo Mu'alla alianza kusema: "Je hivyo inawezekanaje?" Basi Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. akamjibu, uwe na hofu ya Allah swt, uwe daima ukimwona yeye katika mawazo yako, kwa hiyo yeye atakifanaya kila kitu kiwe kikikuogopa wewe, na vile vile kitakuwa kikikuwazia wewe na kukujali wewe. Ewe Mu'alla ili kujipatia mapenzi ya Allah swt lazima uwatendee watu matendo mema, na utambue wazi wazi kuwa Allah swt anapendezewa sana na moyo wa ukarimu na huchukizwa sana na ubahili na huwa na uadui nao.


Angalia ! Wewe kama utaniomba chochote na mwisho wake wewe ukaaza kufanya mapenzi nami, na badala yake mimi nitafurahishwa sana iwapo wewe hautaniomba chochote na hautapata chochote kutoka kwangu na baada ya hayo wewe bado ukawa na mapenzi nami. Na kwa hakika ukiniuliza mema yote naweza kuyafanya kwa ajili yako basi ukweli ni kwamba sifa zote ni za Allah swt kwa sababu yeye amekupitishia neema yake kwa mikono yangu mimi nimekuwa ni kipitishio tu kwa ajili yako kwa hiyo yeye ndiye anayestahiki sifa zote." "Kwa kusikia hayo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. alimwambia, "Nyamaza!" Wale mafukara ambao wanawajali ndugu na jamaa zao na kuwawia wema wenzao, Allah swt huwapa ujira mzuri sana, kwa sababu Allah swt amesema katika Qur'an Tukufu: Surah Sabaa, 34, ayah 37: Na si mali yenu wala watoto wenu watakao kukaribisheni kwetu muwe karibu, isipo kuwa aliye amini na akatenda mema. Hao basi watapata malipo maradufu kwa walio yafanya. Nao watakuwa salama katika maghorofa.. Sheikh Quleyni amenakili riwaya kutoka kwa Ahmad bin 'Isa kuwa Allah swt amesema katika Qur'an Tukufu, Surah Al Maida, 5, Ayah 55: Hakika rafiki yenu mlinzi ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini, ambao hushika Sala na hutoa Zaka nao wananyenyekea . Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema kuwa kwa neno 'Innama' inamaanisha kuwa katika kazi zenu au shughuli zenu zote, mwenye kuwa na haki zaidi kuliko yeyote juu ya nafsi zenu na mali zenu ni Allah swt, baada yake ni Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na baada yake ni, Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. na hadi kufikia Qiyama Maimamu a.s. kutokea kizazi chake.


Vile vile Allah swt ameelezea fadhila zao kwa kusema Qur'an Tukufu, Surah Al Maida, 5, Ayah 55: Hakika rafiki yenu mlinzi ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini, ambao hushika Sala na hutoa Zaka nao wananyenyekea Kisa katika ayah hii ni kwamba Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. alikuwa akisali sala ya Dhuhuri, alipomalizia raka'a ya pili tu akatokezea mwombaji. Siku hiyo Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. alikuwa amevaa Khullah yenye thamani ya Dirham elfu moja ambayo alikuwa amepewa zawadi na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. Na Imam a.s. alipokuwa katika hali ya Ruku'u, kulitokezea maskini mmoja ambaye akasema, "Ewe Walii wa Allah swt na muumin halisi, iwe salamu juu yako, naomba unipe mimi maskini sadaka yoyote. Kwa hayo Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. aliinamisha chini Hulla na kwa ishara akamwambia huyo maskini aichukue."


Kwa tukio hili ndipo Allah swt alipoteremsha ayah hii kwa ajili yake na kwa ajili ya kizazi chake na kuonyesha fadhila na kufuzu kwao. Fadhila zao kuwa wanagawa sadaka hata kama watakuwa katika hali ya Rukuu. Kwa hakika imekuja kujulikana kuwa yule maskini aliyekuja kuomba alikuwa si mtu bali alikuwa ni Malaika ambaye alikuja kuomba, na vile vile katika kizazi kizima cha Maimam a.s. pia tumeona mara nyingi sana Malaika huwa wanakuja kuomba katika sura ya maskini. . Katika kitabu kiitwacho Ihtijaj humo Tabarasi amenakili riwaya kutoka Al Imam Muhammad al-Baquir a.s. kuwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ameelezea kuhusu ayah hiyo kuwa: "Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. katika hali ya sala akiwa katika Ruku'u alitimiza wajibu wake na akatoa Zaka na Allah swt ndipo alipoiteremsha hiyo ayah na makusudio yake yalikuwa ni kupata ridhaa ya Allah swt."


. Ali bin Ibrahim katika kitabu chake Tafsir ananakili riwaya kutoka kwa baba yake Ma'arifat Safwan kuwa Al Imam Muhammad al-Baquir a.s. amesema: "Siku moja Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alipokuwa amekaa pamoja na 'Abdullah bin Salam kulikuwa na kikundi cha Mayahudi pia. Na wakati huo ikateremshwa ayah ya Qur'an Tukufu, Surah Al Maida, 5, Ayah 55: Hakika rafiki yenu mlinzi ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini, ambao hushika Sala na hutoa Zaka nao wananyenyekea

Baada ya hapo mara Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akatoka nje haraka na akaelekea msikitini na huko njiani alikutana na mwombaji mmoja na hivyo Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwuliza: "Je kuna mtu aliyeweza kukusaidia?" Basi huyo mwombaji akasema, "Naam, kuna mtu anayesali msikitini humo ndiye aliyenisaidia." Na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alivyoukaribia msikiti akamwona huyo mtu si mwingine bali ni Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. Na riwaya hii vile vile imenakiliwa na Abu Hamza ambaye ameandika katika Tafsir Ayyashi.